Muhammadu Buhari, rais wa zamani wa Nigeria afariki dunia Uingereza alikokuwa matibabuni
Muhammadu Buhari, rais wa zamani wa Nigeria aliyewahi pia kuitawala nchi hiyo kijeshi amefariki dunia mjini London, Uingereza alikokuwa kipatiwa matibabu akiwa na umri wa miaka 82.
Buhari, ambaye alijaribu mara tatu bila mafanikio kuwania kiti cha urais katika chaguzi za kidemokrasia nchini Nigeria, hatimaye alipata ushindi wa kihistoria mwaka 2015, na kuwa mgombea wa kwanza wa upinzani nchini humo kushinda.
Mnamo 2019, Buhari alichaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka minne.
Katika Nigeria iliyokuwa ikishuhudia kila mara tawala mbalimbali za kijeshi zilizoingia madarakani kupitia mapinduzi, mwishoni mwa 1983 kulitokea mapinduzi mengine dhidi ya Rais mteule Shehu Shagari; na Buhari, ambaye wakati huo alikuwa meja jenerali, akawa mtawala wa kijeshi wa nchi hiyo.
Buhari alitawala kwa muda wa miezi 20, kipindi ambacho kinakumbukwa kwa kampeni dhidi ya utovu wa nidhamu na ufisadi, pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Takribani wanasiasa 500, maafisa na wafanyabiashara walifungwa jela kama sehemu ya kampeni dhidi ya ubadhirifu na ufisadi.
Muhammadu Buhari alizaliwa Desemba 1942 huko Daura katika jimbo la Katsina kaskazini mwa Nigeria, karibu na mpaka na Niger. Wakati huo, Nigeria ilikuwa inadhibitiwa na Waingereza.
Baba yake Buhari, ambaye alifariki wakati yeye akiwa na umri wa miaka minne, alikuwa kutoka jamii ya Fulani, wakati mama yake, ambaye ndiye aliyemlea, alikuwa kutoka jamii ya Kanuri.../