Russia yaonya US, waitifaki: Msiitishie Russia na Korea Kaskazini
Moscow imeionya Marekani na waitifaki wake dhidi ya kuzitishia Russia na Korea Kaskazini.
"Moscow inazionya Marekani, Korea Kusini na Japan dhidi ya kutumia uhusiano wao kama chombo cha kuzilenga Russia na Korea Kaskazini," Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema katika mkutano na waandishi wa habari kufuatia mazungumzo na mwenzake wa Korea Kaskazini, Choe Son Hui huko Wonsan.
"Uongozi wa Korea Kaskazini ulifanya hitimisho muhimu muda mrefu kabla ya Israel na Marekani kuishambulia Iran," amesema akijibu swali linalohusiana na kadhia hiyo.
Ameeleza bayana kuwa, "Hitimisho hili lilifanywa kwa wakati mwafaka, na hakuna anayefikiria kutumia mabavu dhidi ya Korea Kaskazini licha ya kuongezeka uwepo wa kijeshi wa Marekani, Korea Kusini na Japan nchini kote."
Lavrov amebainisha kuwa,"Tunaonya dhidi ya kutumia mahusiano haya ili kujenga ushirikiano dhidi ya mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na Korea Kaskazini na, bila shaka, Russia."
Ikumbukwe kuwa, utawala wa Kizayuni ulianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran tarehe 13 Juni na kuyashambulia maeneo ya kijeshi, ya nyuklia na makazi ya raia wa Jamhuri ya Kiislamu kwa muda wa siku 12.
Marekani iliingilia kati na kufanya mashambulizi ya kijeshi katika maeneo matatu ya nyuklia huko Natanz, Fordow na Isfahan hapa nchini Iran tarehe 22 Juni. Vikosi vya jeshi la Iran hata hivyo vilifanya mashambulizi makali ya kujibu mapigo mara baada ya uvamizi huo.