Gaza inahusiana vipi na janga la Srebrenica?
Katika mwaka wa 30 wa kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya Srebrenica, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika ujumbe wake akisema: "Lau dunia ingejifunza kutokana na janga hilo, tusingeshuhudia mauaji mengine ya kimbari dhidi ya Waislamu hii leo, na mara hii huko Gaza."
Sentensi hii fupi ya Sayyid Abbas Araqchi inabeba ukweli mchungu zaidi wa zama hizi. Ukweli huo unaonyesha kwamba, irada ya kisiasa inayotawala dunia ya sasa imewezesha uhalifu huo kurudiwa tena na tena.
Akiashiria uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuiteua Julai 11 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari ya Srebrenica," Araqchi ameitaja siku hiyo kuwa ni ukumbusho wa aibu kwa wale ambao ama walihusika katika uhalifu huo wa kutisha, au kwa ukimya wao, walifungua njia ya mauaji ya maelfu ya Waislamu wasio na hatia."

Mnamo Julai 11, 1995, Vita vya Bosnia vilifikia kilele cha ukatili wa kutisha. Mji wa Srebrenica, uliotangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa "eneo salama" kwa raia Waislamu, ulitekwa na wanamgambo wabaguzi wa rangi wa Kiserbia wakiongozwa na Ratko Mladic. Waserbia wapatao elfu mbili wenye fikra za kibaguzi na wauaji, walitenganisha zaidi ya wanaume na wavulana elfu 8 wa Kiislamu wa Bosnia kutoka kwenye familia zao, wakawahamishia kwenye kambi za muda na kuwauwa kwa umati, kwa sababu tu ya dini na mbari zao. Haya yalifanyika kwa mpangilio maalumu mbele ya macho ya ulimwengu usiojali na mbele ya wanajeshi wa Kofia Bluu wa Umoja wa Mataifa kutoka Uholanzi. Mauaji hayo yalifanywa kwa ustadi sana kiasi kwamba, hata makaburi ya wahanga Waislamu wa Bosnia yalihamishwa mara kadhaa ili kuficha ukweli. Serikali za nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani, licha ya kujua azma ya Waserbia ya kufanya mauaji ya kimbari, sio tu kwamba zilijizuia kuzuia uhalifu huo, lakini pia, kwa ukimya wao, zilihusika katika jinai hiyo ya kutisha. Wabaguzi wa Kiserbia waliwaua kikatili zaidi ya watu laki moja (100,000) wakati wa Vita vya Bosnia kuanzia 1992 hadi 1995. Zaidi ya watu milioni 2 walikimbia makazi yao, na wanawake na wasichana 50,000 walibakwa kwa zamu kwenye kambi za wakiimbizi.
Mnamo mwaka 1995, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alisema baada ya janga la Srebrenica kwamba: "Huku ni kushindwa kwa jamii ya kimataifa." Leo, Antonio Guterres, anaongoza umoja huo ambao hadi sasa umeshindwa kutekeleza maazimio tisa ya kusitisha mauaji yanayofanywa na Israel huko Gaza kutokana na kura za turufu za Marekani.
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa, asilimia 93 ya watoto wa Gaza wanasumbuliwa na uhaba wa chakula; takwimu inayokumbusha mzingiro wa Srebrenica. Kilichoifanya Srebrenica kuwa tukio la kimataifa sio tu ukubwa wa maafa yake, bali ni kutochukua hatua za kukabiliana na uhalifu huo jamii ya kimataifa chini ya ushawishi wa serikali za nchi za Magharibi. Mwenendo huu unarudiwa hii leo, tena kwa uwazi na kwa undani zaidi, katika Ukanda wa Gaza.
Kutumia njaa kama silaha ya vita, kulazimishwa watu kuhama makazi yao, kunyimwa huduma za msingi, na mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia ni mifano inayotambulika ya mauaji ya kimbari chini ya Mkataba wa 1948. Kwa msingi huo, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilionya rasmi Januari 2024 kwamba kuna hatari ya kutokea mauaji ya kimbari huko Gaza na kwamba Israel inalazimika kuchukua hatua za kuyazuia. Hata hivyo hukumu hiyo, kama yalivyokuwa maonyo mengi kama hayo kuhusu Srebrenica, haikupewa uzito, na kinyume chake nchi za Magharibi zimeisaidia Israel kuendeleza uhalifu kwa kuipatia silaha, kubuni simulizi za vyombo vya habari, na msaada wa kidiplomasia.
Ukweli ni kwamba mauaji ya kimbari sio tu ni janga la binadamu, lakini pia ni ishara ya kuporomoka maadili ya mfumo wa kimataifa ambao hauheshimu tena haki za binadamu, kutambua haki, au hata kuamini jukumu na wajibu wa kulinda maisha ya raia. Wahanga wa Srebrenica waliachwa wafe peke yao kwa ahadi hewa za kudhaminiwa usalama. Hii leo, Gaza inaangamizwa kwa ahadi hewa za "suluhisho la serikali mbili."
Srebrenica ni nembo ya upuuzaji na kutochukua hatua madola makubwa duniani mkabala wa maafa ya binadamu. Lakini Gaza ni nembo ya ushiriki wa kisasa katika mauaji ya kimbari. Tofauti kubwa iliyopo baina ya ukatili unaofanyika Gaza na ule wa Srebrenica ni kwamba huko Bosnia, baada ya vita kumalizika, nchi za Magharibi ziliingilia kati kujenga upya, kuanzisha mahakama ya kushughulikia uhalifu iliiofanyika, kutambua makaburi ya umati, na kurekodi simulizi za waathiriwa. Lakini huko Gaza, hata kuwaonea huruma waathiriwa na kutangaza mshikamano na watu wa eneo hiilo kunatambuliwa katika miji mikuu ya nchi Magharibi kuwa uhalifu. Hata kusema neno "mauaji ya kimbari" humfanya mtu akabiliwe na shutuma za kuwa na chuki dhidi ya Wayahudi, na wito wowote wa kusitishwa uhalifu huo unatafsiriwa kuwa ni kuunga mkono ugaidi!

Nchi za Magharibi zinazodai kutetea ubinadamu hazijachukua hatua yoyote ya kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanyika waziwazi na mbele ya macho ya walimwengu.