Russia yakadhibisha madai ya Axios kuhusu urutubishaji urani wa Iran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema madai ya tovuti ya habari ya Marekani ya Axios kwamba Rais Vladimir Putin wa Russia ameiomba Iran isirutubishe madini ya uranium kuwa "kampeni chafu ya kisiasa" .
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa taarifa ikikanusha ripoti ya tovuti ya Axios iliyodai kwamba Russia imeitaka Iran isimamishe kikamilifu urutubishaji wa urani hadi kiwango cha asilimia sifuri.
Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeielezea ripoti hiyo ya Axios kuwa ni "kampeni chafu ya kisiasa."
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imebainisha kuwa inawezekana kukisia tu ni nani aliyetoa agizo hilo mara hii, lakini moja ya machapisho ya karibuni zaidi, lenye anuani ya "Putin atoa wito kwa Iran ikubali makubaliano inayotaka Marekani, yanayomaanisha urutubishaji hadi kiwango cha sifuri," linaonyesha uwezekano mkubwa wa kuwepo kampeni nyingine chafu ya kisiasa iliyoanzishwa kwa lengo la kushadidisha mvutano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Wizara hiyo imebainisha kuwa: Moscow imekuwa ikisisitiza mara kwa mara ulazima wa kutatua mgogoro unaohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran kupitia njia za kisiasa na kidiplomasia tu na imeeleza utayarifu wake wa kusaidia kupatikana njia za ufumbuzi zinazokubalika.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imemalizia taarifa yake kwa kusema: "tunatoa wito kwa vyombo vya habari vya kimataifa vinavyowajibika kutegemea vyanzo rasmi vya habari, kuchunguza kwa kina suala hilo, na si kueneza habari za uongo".../