Qalibaf: Waisraeli wasiopungua 500 waliangamizwa katika vita na Iran
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Baqer Qalibaf amesema kusitishwa kwa uvamizi wa kijeshi wa hivi karibuni wa Israel dhidi ya Iran kulitokana na kushindwa kwa utawala huo, na wala sio kutokana na kujizuia kwa upande wake.
Katika mahojiano ya moja kwa moja akizungumzia vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na muungano wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, Qalibaf amesema idadi ya Waisraeli waliouawa na kujeruhiwa katika majibu ya Iran kwa uchokozi na uvamizi huo ni kubwa zaidi ya ripoti rasmi zilizotolewa.
Amerejelea mifano ya kisayansi inayoonyesha kuwa, kwa kila idadi ya majeruhi 3,500 inayoripotiwa, inapaswa kwenda sanjari na angalau vifo 500, akisisitiza kuwa, "iwapo waliojeruhiwa ni 3,500, inamaanisha angalau 500 walikufa."
Spika Qalibaf ameeleza bayana kuwa, Iran ilikabiliana sio tu na Israel, bali na shirika la kijeshi la Wamagharibi NATO na madola ya Magharibi chini ya amri ya Marekani.
Amesisitiza kuwa, uwezo wa Iran katika ardhi na anga ulichangia kushindwa kwa utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa, "Tumevilemaza vituo vya kijeshi na kiulinzi vya Israel."
Kabla ya hapo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza kuwa, jibu la Iran kwa utawala wa Kizayuni katika makabiliano ya hivi majuzi lilikuwa kali na la kuponda, kwani utawala huo ghasibu haujawahi kupata jibu kama hilo katika historia yake yote isiyo halali.