Afrika imenakili vifo 4,200 vya kipindupindu na mpox 2025
Afrika imerekodi vifo zaidi ya 4,200 kutokana na miripuko ya kipindupindu na mpox inayoendelea kuripotiwa katika maeneo tofauti ya bara hilo mwaka 2025, Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) kimesema.
Yap Boum II, Naibu Mkurugenzi wa miripuko ya mpox katika taasisi ya Africa CDC amesema kipindupindu na mpox ni miongoni mwa miripuko mikubwa ya magonjwa iliyoripotiwa hadi sasa mwaka huu 2025, ambapo imesababisha vifo vya watu 4,275 tangu mwanazoni mwa mwaka huu.
Takwimu kutoka kwa wakala maalum wa huduma za afya wa Umoja wa Afrika zilionyesha kuwa, tangu kuanza kwa mwaka huu, nchi 21 za Afrika zimerekodi kesi 176,136 zinavyoshukiwa kuwa za kipindupindu, na vifo 3,697 vinavyohusiana na maradhi hayo.
Uhaba wa maji safi na salama umebainishwa kuwa chanzo kikuu cha mripuko wa mara kwa mara wa kipindupindu barani Afrika, ambao unachangiwa zaidi na mifumo mbovu ya afya, huku bara hilo likikabiliwa na miripuko ya magonjwa na dharura za afya ya umma.
Kulingana na Afrika CDC, nchi 23 za Afrika pia zimerekodi visa 79,024 vya ugonjwa wa mpox na vifo 578 vinavyohusiana na ugonjwa huo tangu kuanza kwa mwaka huu 2025.
Mnamo Agosti mwaka jana, Afrika CD ilitangaza mripuko wa mpox kuwa dharura ya afya ya umma ya usalama wa bara hilo.
Muda mfupi baadaye, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza ugonjwa huo wa virusi kama dharura ya afya ya umma ya kimataifa.