Mapigano makali yazuka upya magharibi mwa mji mkuu wa Libya
Mapigano makali yamezuka upya katika eneo la Janzour, yapata kilomita 12 magharibi mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, kati ya makundi hasimu yenye silaha ambayo yako chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ya Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.
Vyombo vya habari vya ndani ya Libya vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mapigano yalianza wakati Kikosi cha Mahmoud Boujaafar kilipovamia makao makuu ya Brigedi ya Sita inayoongozwa na Munir Al-Sweih na kusababisha majibu ya mashambulizi yalizusha vita vikali ambavyo ndani yake silaha za kati na nzito zimetumika.
Barabara kuu ya pwani ya kuelekea Zawiya na soko kuu la mboga zilifungwa, na vikosi vya kijeshi vilitanda kila mahali.
Kuzuka mapigano hayo kunaonesha udhaifu wa makubaliano ya kiusalama yaliyotiwa saini wiki iliyopita kati ya GNU na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Ghasia (Radaa). Makubaliano hayo yalijumuisha kuondoka askari wa Radaa kwenye kambi ya kikosi cha anga ya Mitiga. Kipengee kingine kilihusiana na uteuzi wa mkuu mpya wa Polisi wa Mahakama, kukabidhiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali watu wanaosakwa na mambo mengine kadhaa.
Libya bado imegawanyika kati ya serikali mbili, moja ni ya Umoja wa Kitaifa GNU inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa inayotawala upande wa magharibi na nyingine ni serikali hasimu inayotawala upande wa mashariki mwa Libya ikiongozwa na Osama Hammad. Kuna mikono mingi ya nje inayochochea machafuko huko Libya. Serikali ya Osama Hammad inaungwa mkono na Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.