Pezeshkian: Jithada za kuzuia uhusiano mwema kati ya nchi za Kiislamu hazitafanikiwa
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria jitihada za maadui za kuzusha hitilafu na mgawanyiko baina ya nchi za Kiislamu; na kushindwa kuasisiwa uhusiano wenye matunda katika eneo hasa kati ya Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.
Amesema kuwa,jitihada za maadui hazitazaa matunda kutokana azma na irada waliyonayo viongozi wa ulimwengu wa Kiislamu na vile vile viongozi wa ngazi za juu wa Iran na Azerbaijan ya kupanua uhusiano na ushirikiano kati yao.
Rais Pezeshkian amebainisha haya katika mkutano aliofanya na ujumbe wa ngazi ya juu ulioongozwa na Shahin Mustafayev Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan ulioko ziarani hapa Tehran.
Pezeshkian ameutaja uhusiano kati ya nchi mbili kuwa wa kirafiki kwa mujibu wa mafungamano ya kiutamaduni na kidini kati ya serikali na mataifa haya mawili.
"Tuna nia ya kupanua mahusiano haya katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Hakuna vikwazo katika njia ya kupanua uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili", amesema Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika mazungumzo hayo na ujumbe wa ngazi ya juu wa Azerbaijan hapa Tehran, Rais wa Iran ameashiria pia ziara yake ya karibuni katika Jamhuri ya Azerbaijan na mazungumzo chanya pamoja na makubaliano yaliyofikiwa na maafisa wa ngazi ya juu wa Iran na Azerbaijan na kusema: " Tunaamini kuwa iwapo uwezo mkubwa na suhula nyingi ilizonazo Iran na Jamhuri ya Azerbaijan zitatumiwa kupanua ushirikiano,hatua hiyo itakuwa kwa maslahi na manufaa mapana ya nchi hizo mbili rafiki na ndugu.
Shahin Mustafayev Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan alikutana pia na Ali Larijani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.