Jumatatu 22 Septemba
Leo ni Jumatatu 29 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1447 Hijria Qamaria, mwafaka na tarehe 31 Shahrivar 1404 Hijria Shamsia mwafaaka na tarehe 22 Septemba 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1688 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Septemba mwaka 337, vilianza vita vya miaka 13 kati ya Iran na Roma katika utawala wa Shapur II (Dhul Aktaf), wa silsila ya watawala wa Sasani na ambavyo katika historia vilifahamika kama vita vya duru ya kwanza. Vita vya duru ya pili vilianza mwaka 359, ambapo katika duru zote, Wairani waliibuka na ushindi. Katika duru ya kwanza ambapo vita hivyo vilidumu hadi mwaka 350, Waroma walipoteza kila kitu walichokuwa wakikidhibiti eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterranean, na mfalme wao aliuawa katika duru ya pili ya vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein yalianza kufanya mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vikawa vimeanza. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.
Hatimaye, jeshi la uvamizi la utawala wa Saddam, baada ya kushindwa mara kwa mara na vikosi vya Kiislamu vya Iran, lililazimika kurudi nyuma hadi kwenye mipaka inayotambuliwa kimataifa. Mnamo tarehe 29 Mordad 1367 Hijria ya jua (sawa na Agosti 20, 1988), kwa mujibu wa Azimio la Umoja wa Mataifa nambari 598, makubaliano ya kusitisha vita kati ya nchi hizo mbili yalifikiwa.
Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kila mwaka katika kumbukumbu ya kuanza kwa uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran mnamo tarehe 31 Shahrivar 1359 Hijria ya jua (sawa na Septemba 22, 1980), hufanyika maadhimisho ya wiki nzima kwa jina la "Wiki ya Ulinzi Mtukufu" kwa heshima ya kujitolea kwa taifa la Kiislamu la Iran katika kukabiliana na uvamizi huo.

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 22 Septemba 1979, Allama Abul A‘la Maududi, mwanafikra na msomi mashuhuri wa Kiislamu kutoka Pakistan, alifariki dunia. Maududi alizaliwa mwaka 1903 katika mji wa Aurangabad, na aliendeleza masomo yake ya juu katika fani za elimu ya dini. Mnamo mwaka 1932, kwa usaidizi na ushirikiano wa kundi la marafiki zake, alianzisha jarida maarufu Tarjuman al-Qur’an huko Hyderabad, Pakistan. Aidha, alihudumu kwa muda kama mmoja wa walimu mashuhuri katika taasisi ya Kiislamu ya Dar al-Salaam katika eneo hilo.
Allama Maududi alitambuliwa kama mmoja wa wanafikra wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu na miongoni mwa maulamaa mashuhuri wa Bara Hindi. Alikuwa mwasisi wa harakati za kupinga dhulma na ubeberu miongoni mwa maulamaa wa eneo hilo. Mnamo mwaka 1941, alianzisha chama cha Jamaat-e-Islami kwa lengo la kuunda muungano imara wa kisiasa wa Kiislamu kati ya wananchi na maulamaa wa Pakistan.
Chama cha Jamaat-e-Islami kilikuwa taasisi ya kwanza ya kisiasa na ya Kiislamu yenye muundo thabiti katika historia ya Pakistan, na kilicheza nafasi muhimu katika kuwaelimisha wananchi, kuwaongoza kiroho, na kufichua sura ya kweli ya itikadi ya Wahabi nchini humo. Mnamo mwaka 1953, Maududi alikamatwa na kufungwa gerezani kwa kuandaa maandamano dhidi ya makundi ya Qadiani na Wahabi, yaliyotajwa kuwa ya upotovu.
Allama Maududi aliacha nyuma zaidi ya machapisho mia moja ya kisiasa na Kiislamu. Alikuwa miongoni mwa wasomi wa kwanza wa Kiislamu waliyotangaza kwa uwazi na kwa msimamo thabiti kuunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ndani ya Pakistan. Hatimaye, msomi huyu mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia tarehe 22 Septemba 1979 akiwa na umri wa miaka 76 katika mji wa Lahore.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa na uliong'ara. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.

Katika siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, nchi ya Bulgaria ilijipatia uhuru kutoka kwa utawala wa Othmania. Bulgaria ilianza kutawaliwa na utawala huo mwishoni mwa karne ya 14. Wakati huo maudhi dhidi ya Wakristo yalianza na kuendelea kwa karibu miaka 500 ya udhibiti wa Othmania kwenye nchi hiyo na suala hilo liliibua uasi wa mara kwa mara wa raia wa Bulgaria. Hatimaye mwaka 1878 nchi hiyo ilipata uhuru na kujitangazia mamlaka ya ndani. Tarehe 22 Septemba mwaka 1908 mfalme wa wakati huo wa Bulgaria alitangaza uhuru kamili wa nch hiyo.
