Feb 22, 2026 02:17 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili mwezi 4 Ramadhani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 22 Februari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 871 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Muhammad maarufu kwa jina la Ibn Khorasani, mtaalamu wa elimu ya Nahw, malenga na mwandishi wa Baghdad. Ibn Khurasani alizaliwa mwaka 494 Hijria huko Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran. Msomi huyo baadaye alielekea Baghdad, Iraq na kuishi katika mji huo. Muhammad bin Muhammad alihitimu masomo kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Ibn Khurasan ameandika mashairi mengi ambayo mengi kati ya hayo yamepotea. ***

Katika siku kama ya leo miaka 839 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria aliaga dunia Abul-Qassim, Hibbatullah bin Jaafar, mwanafasihi na mshairi mashuhuri wa Kimisri. Msomi huyo ambaye alijulikana pia kwa lakabu ya Kadhi Said ibn Sanai al-Mulk alizaliwa huko Cairo Misri mwaka 545 Hijria katika familia ya Kiislamu. Alijifunza Qur’ani na elimu ya Nahw katika mji wa Cairo na kusoma elimu ya hadithi na elimu nyingine huko Alexandaria nchini Misri kwa walimu mahiri wa zama hizo. Ibn Sanai al-Mulk alionyesha kipaji na umahiri mkubwa katika uga wa utunzi wa mashairi na fasihi akiwa katika rika la ujana. Miongoni mwa athari zake ni diwani ya mashairi ambayo ina madhumuni mbalimbali ambapo ndani yake mnapatikana pia beti za mashairi zinazoelezea tukio la Ashura na kuuawa shahidi kidhulma Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). ***

Katika siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Isfand mwaka 1299 Hijria Shamsia, Uingereza ilitekeleza siasa zake za kikoloni kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran. Njama hiyo ya mapinduzi ilipangwa na maafisa wa serikali ya Uingereza waliokuwa mjini Tehran wakishirikiana na baadhi ya maafisa usalama wa mji huo. Wafanya mapinduzi waliudhibiti mji mkuu baada ya mapigano ya muda mfupi, na Ahmad Shah Qajar akalazimika kumteua Reza Khan kuwa Kamanda Mkuu wa majeshi. Miaka minne baadaye Reza Khan ambaye alikuwa akiungwa mkono na kusaidiwa sana na Waingereza kutokana na kukandamiza harakati za ukombozi za wananchi alifanywa mfalme wa Iran hadi mwaka 1320 Hijria Shamsia, ambapo aliondolewa madarakati na Waingereza wenyewe na kupelekwa uhamishoni baada ya kuegemea upande wa Ujerumani katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. 

Siku kama hii ya leo miaka 68 iliyopita aliaga dunia Abul Kalaam Ahmad Azad, aalim, khatibu hodari na mwanasiasa wa India akiwa na umri wa miaka 70. Abul Kalaam Azad alianzisha harakati za kisiasa dhidi ya ukoloni wa Uingereza na kwa lengo la kuwaamsha Waislamu wa India akiwa na umri wa miaka 17. Mwanasiasa huyo aliwekwa gerezani mara kadhaa kutokana na kuchapisha makala na kutoa hotuba zenye kufichua njama za wakoloni wa Kiingereza. 

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo oparesheni ya kijeshi ya "Khaybar" ilianza wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Oparesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji jasiri wa Iran. Oparesheni hiyo ambayo ilianza kutekelezwa katika eneo la Hurul Huwaizah huko kusini magharibi mwa Iran, wapiganaji wa Kiirani walivuka maji na vinasamasi na kukiteka nyara kisiwa chenye utajiri wa mafuta cha Majnuun karibu na mji wa Basra kusini mashariki mwa Iraq. Mbinu tata za kijeshi zilizotumika katika oparesheni hiyo ya majini na nchi kavu ya Khaibar ziliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi duniani.   

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita miripuko mikubwa ya mabomu ilitokea katika haram mbili tukufu za Maimamu Hadi na Hassan al Askari (as) huko katika mji wa Samarra, kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq na kusababisha hasara kubwa katika eneo hilo tukufu la Waislamu. Uharibifu mkubwa uliosababishwa na miripuko hiyo katika haram hizo tukufu uliwakasirisha Waislamu duniani na hasa wa wafuasi wa madhehebu ya Shia. Maimamu hao wawili ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw).