Kwa nini Tel Aviv inaogopa kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina?
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limejiweka kwenye hali ya tahadhari kukabiliana na matukio yanayoweza kutokea baada ya baadhi ya nchi za Magharibi kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina.
Redio ya jeshi la Israel imetangaza katika ripoti yake kwamba: Makamanda wa kijeshi wa Israel wametuma batalioni nane katika Ukingo wa Magharibi wakati huu ambapo leo Jumatatu tarehe 22 Septemba, ndiyo siku ambayo baadhi ya nchi za Magharibi ziliahidi kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina.
Zaidi ya nchi 10 za Magharibi zilitangaza kuwa zitaitambua Palestina kama taifa huru katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Jumatatu. Tel Aviv, kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, imetishia kujibu hatua hiyo kwa kuuteka na kuukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Canada, Australia, Ureno, Ubelgiji, Malta, Luxemburg, San Marino, Andorra na Ufaransa ni miongoni mwa nchi ambazo zimetangaza kuwa zitaitambua Palestina katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Palestina kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Huku vita vya Ghaza vikiendelea na utawala wa Kizayuni ukishikilia kuendeleza ukatili na mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina wanaoishi Ghaza, fikra za walio wengi duniani nazo zimezidi kuwa dhidi ya utawala wa Kizayuni. Kufanyika maandamano makubwa katika nchi mbalimbali duniani kupinga jinai za Israel na mauaji yake ya umati huko Ghaza sambamba na kuenea picha za kusikitisha zinazoonesha jinsi watu wanavyoatilika kwa njaa na kiu huko Ghaza hususan katika miezi ya hivi karibuni, kumeongeza mashinikizo ya walimwengu dhidi ya viongozi wa nchi mbalimbali za Ulaya. Viongozi wa nchi za Ulaya ambao daima wamekuwa wakidai kutetea haki za binadamu na kuheshimu uhuru wa mtu binafsi na wa kijamii, wamelazimika katika miezi ya hivi karibuni kujionesha kwa watu kuwa wameacha moja kwa moja kuiunga mkono Israel na wanaonekana wakilaani angalau kwa maneno, jinai za Wazayuni dhidi ya wakazi wa Ghaza. Kwa hakika silaha za maangamizi makubwa ya umati zinazotumiwa na utawala wa Kizayuni yakiwemo mabomu ya fosforasi nyeupe, mashambulizi dhidi ya maeneo yaliyotangazwa na Israel na Marekani kuwa ni maeneo salama, kufungwa njia za kuwafikishia chakula na dawa wakazi wa Ghaza na uharibifu mkubwa wa miundombinu kama vile mifumo ya maji safi, mahospitali na vituo vya matibabu, ni mambo ambayo yamewaondolea viongozi wa nchi za Ulaya kisingizio chochote cha kuendelea kuiunga mkono Israel. Wakazi wengi wa nchi za Ulaya hivi sasa hawakubali tena kitendo chochote cha kuitetea na kuiunga mkono Israel.
Nchi nyingi za Ulaya zinaamini kwamba ni kwa kuanzishwa taifa huru la Palestina tu na kutambuliwa rasmi haki za Wapalestina ndipo patawezekana kulindwa misingi ya amani na usalama wa kudumu kwenye eneo la Asia Magharibi. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kutambuliwa rasmi nchi ya Palestina na nchi za Magharibi si tu ni kitendo cha kuheshimu haki za binadamu, bali pia ni juhudi za kidiplomasia za kuweka mizani katika siasa za kimataifa.
Sasa, utawala wa Kizayuni unaogopa sana kutambuliwa nchi huru ya Palestina. Moja ya sababu muhimu zaidi ni kwamba kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina, ni tishio kwa kile kinachoitwa uhalali wa utawala wa Kizayuni wa kuvamia na kuteka ardhi yoyote ile. Hadi sasa utawala wa Kizayuni umekuwa ukikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kukiuka haki zao, ukitumia maneno kama vile "haki ya kujilinda," lakini kutambuliwa nchi huru ya Palestina kunapingana na uhalali huo iliyojipa Israel na kunaweza kuongeza mashinikizo ya kimataifa ya kukomesha uvamizi na kutoheshimiwa haki za Wapalestina.

Zaidi ya hayo, makubaliano kama ya Oslo na mazungumzo mengine ambayo yamekuwa yakiunufaisha utawala wa Kizayuni, hivi sasa yanakabiliwa na tishio la kusambaratika kwa kutambuliwa nchi huru ya Palestina.
Kutambuliwa Palestina kunaweza pia kusaidia kuimarisha nafasi ya Wapalestina katika uga wa kimataifa. Iwapo Palestina itatambuliwa kuwa nchi huru, Wapalestina wataweza kushiriki katika mikutano ya kimataifa nakwenye mashirika makubwa duniani sambamba na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa na hivyo kupata fursa ya kutetea haki zao kama nchi huru. Hilo linaweza kuongeza mashinikizo kwa Israel na hatimaye kapatiwa ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Palestina jambo ambalo ni pigo kwa Israel.
Hata hivyo, kutambuliwa rasmi nchi ya Palestina ni hatua ya awali tu inayoweza kufungua njia ya mabadiliko ya kimsingi katika mchakato wa amani na usalama magharibi mwa bara la Asia. Aidha jambo hilo lina changamoto na matatizo mengi, kiasi kwamba haijulikani kama nchi za Ulaya zitaendelea kushikilia msimamo wao wa kuitambua nchi huru ya Palestina au la kutokana na ushawishi na mashinikizo ya dola la kiistikbari la Marekani.