Iran: Ulimwengu unawajibika kukabiliana na ukiukaji wa haki za binadamu wa Israel
-
Abbas Araqchi na Mirjana Spoljaric Egger
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa jamii ya kimataifa inawajibika kukabiliana na hatua za utawala wa Israel za kuendelea kukiuka pakubwa sheria katika eneo la Asia Magharibi.
Abbas Araqchi alieleza hayo jana katika mkutano na Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Mirjana Spoljaric Egger, katika mji wa Geneva, Uswisi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yuko mjini Geneva kushiriki katika duru ya pili ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja na Marekani.
Araqchi amesema kuwa nchi zote zinapasa kufanya juhudi za kulinda misingi ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu.
Ameongeza kuwa utawala wa Israel na Marekani zilikiuka waziwazi haki za binadamu kwa kuua wananchi wa Iran na kushambulia maeneo ya raia na miundombinu wakati wa mashambulizi ya kijeshi ya mwezi Juni mwaka jana.
"Umoja wa Mataifa na mashirika husika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), yana jukumu la kuchukua msimamo wa wazi kuhusu suala hili," amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Kwa upande wake Mirjana Spoljaric amesema kuwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu iko tayari kuimarisha ushirikiano na Iran hususan na Shirika la Mwezi Mwekundu la Iran.
Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu pia amesisitiza umuhimu wa nchi zote kujitahidi kuheshimu kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu.
Mwezi Julai mwaka jana, mwakilishi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu nchini Iran, Vincent Cassard, alitembelea jela ya Evin katika mji wa Tehran kufuatia mashambulizi ya anga ya utawala wa Israel katika jela hiyo yaliyouwa watu 79. Cassard alisema ameshutushwa na mashambulizi hayo ya Israel aliyoyataja kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.