Bandari za miji 60 ya Italia zafungwa ili kuiunga mkono Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i131116-bandari_za_miji_60_ya_italia_zafungwa_ili_kuiunga_mkono_ghaza
Sekta mbalimbali za kiuchumi na huduma katika miji 60 ya Italia, kutoka bandari hadi usafiri wa umma, zimefungwa kwa saa 24 leo Jumatatu kutokana na mgomo wa umma ulioitishwa kwa ajili ya kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina hususan wananchi wa Ghaza.
(last modified 2025-09-22T12:25:21+00:00 )
Sep 22, 2025 12:25 UTC
  • Bandari za miji 60 ya Italia zafungwa ili kuiunga mkono Ghaza

Sekta mbalimbali za kiuchumi na huduma katika miji 60 ya Italia, kutoka bandari hadi usafiri wa umma, zimefungwa kwa saa 24 leo Jumatatu kutokana na mgomo wa umma ulioitishwa kwa ajili ya kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina hususan wananchi wa Ghaza.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars; Italia imeshuhudia mgomo mkubwa wa umma ulioitishwa na chama cha wafanyakazi cha USB na vyama vingine kadhaa leo Jumatatu.

Mgomo huo ulioanza kwa kusitishwa shughuli katika bandari, viwanja vya ndege na shule, umegeuka haraka kuwa jukwaa la kutangaza mshikamano na wananchi wa Palestina huko Ghaza na kupinga sera za serikali ya Italia na Israel za kuendeleza mauaji dhidi ya Wapalestina.

Gazeti la Italia la "Il Giornale" limeripoti kuwa mgomo huo mkubwa uliojumuisha sekta za usafiri, bandari, viwanja vya ndege na elimu, umebeba ujumbe muhimu wa aina mbili, moja ni kutetea haki za wafanyakazi na kijamii ndani ya Italia na pili kulaani jinai za Israel dhidi ya wananchi wa Ghaza.

Washiriki wa mgomo wamesikika wakipaza sauti zao wakisema, Komboa Komboa Palestina! ikiwa ni sehemu ya kupigania ukombozi wa Palestina na kulaani mzingiro na jinai za kinyama wanazofanyiwa wananchi wa Palestina. Maandamano ya nchi nzima yamefanyika katika miji zaidi ya 60 ya Italia, kwa kaulimbi maarufu inayosema: "Kila kitu lazima kisimame... Palestina iko mioyoni mwetu."

Imesemwa kwamba mgomo huo ulikuwa na lengo la kupinga mauaji ya kimbari ya Wapalestina, kukomesha kupelekewa silaha Israel kupitia bandari za Italia na kuchukuliwa hatua za kukomeshwa jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.