EU yagawanyika juu ya kifurushi cha vikwazo dhidi ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i131088-eu_yagawanyika_juu_ya_kifurushi_cha_vikwazo_dhidi_ya_russia
NATO imepeleka ndege tatu za kivita za Ufaransa huko Poland Mashariki kwa kile kilichotajwa kuwa ni sehemu ya kukabiliana na Russia. Wachambuzi wengi wanasema kuwa, ni vitendo kama hivyo vya jeshi la nchi za Magharibi NATO la kutanua uwepo wake karibu na Russia ndivyo vilivyozusha na kushadidisha mgogoro wa Ukraine.
(last modified 2025-09-22T02:44:03+00:00 )
Sep 22, 2025 02:44 UTC
  • EU yagawanyika juu ya kifurushi cha vikwazo dhidi ya Russia

NATO imepeleka ndege tatu za kivita za Ufaransa huko Poland Mashariki kwa kile kilichotajwa kuwa ni sehemu ya kukabiliana na Russia. Wachambuzi wengi wanasema kuwa, ni vitendo kama hivyo vya jeshi la nchi za Magharibi NATO la kutanua uwepo wake karibu na Russia ndivyo vilivyozusha na kushadidisha mgogoro wa Ukraine.

Umoja wa Ulaya umezindua kifurushi chake cha 19 cha vikwazo dhidi ya Russia ambacho kinalenga sekta za nishati, benki na teknolojia ya hali ya juu. Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula Von der Leyen, amesema: "Tunashughulikia suala la kufadhili ulinzi wa Ukraine. Hii ni kwa msingi wa kutaifisha mali zisizohamishika za Russia. Lazima tuwe wazi sana, hivi ni vita  vya Russia, na mhusika lazima alipe."

Lakini ndani ya Bunge la Ulaya, wakosoaji wanaonya kwamba walipa kodi wa nchi za Ulaya ndio wanaoshinikizwa sana na wanaopata madhara na mateso zaidi. Hadi hivi sasa Umoja wa Ulaya umeshatumia Euro bilioni 169 kugharamia vita vya Ukraine wakati ambapo bajeti mpya ya miaka saba imeongeza juu Euro bilioni 100 nyingine. 

Viwanda vya kuzalisha silaha vya Marekani ndiye mshindi pekee wa vita nchini Ukraine kwa sababu licha ya hali ambayo wastani wa uzalishaji wa viwanda vya silaha vya Marekani umeshuka kwa 10% kwa mwaka mzima, lakini bei za hisa za wakandarasi wa masuala ya kijeshi wa Marekani zimepanda.

Viongozi wa serikali 27 wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kupinga mpango wa hivi sasa wa umoja huo wa kuiwekea vikwazo vipya Russia. Hasa kwa kuzingatia kuwa, awamu 19 za vikwazo dhidi ya Russia hazijazaa matunda yaliyotakiwa. Wananchi wa nchi za Ulaya ndio wanaoteseka, Ukraine imesambaratishwa vibaya huku viwanda vya silaha vya Marekani vikizidi kunufaika.