Iran na Pakistan zaja na mkakati wa pamoja wa ustawi wa kiuchumi
Kamisheni ya 22 ya Pamoja ya Uchumi (JEC) kati ya Iran na Pakistan, iliyofanya kikao chake hapa mjini Tehran imetilia mkazo suala la kurejeshwa mkakati wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili jirani.
Mkutano huo umeangazia uwezo mkubwa wa kiuchumi ambao bado haujatumiwa na nchi hizi mbili licha ya kupita miongo kadhaa ya uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara.
Kwa mtazamo wa pamoja wa kustawisha biashara baina ya nchi hizi mbili kutoka kiwango chake cha sasa cha zaidi ya dola bilioni 3 na kuhakikisha kinafikia dola bilioni 10, mataifa hayo mawili sasa yako tayari kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta nyingi na kuweka msingi madhubuti wa kuimarishwa ushirikiano wa kikanda.
Iran na Pakistan zinatambua kuwa viwango vyao vya kibiashara vya sasa haviakisi uwezo halisi wa uhusiano wao wa kiuchumi. Pengo hili halina maana kuwa hakuna fursa za ushirikiano, fursa zipo, kinachokosekana ni kutumiwa vizuri fursa hizo.
Tume hiyo ya pamoja ya kiuchumi ya Iran na Pakistan imetilia mkazo wajibu wa kuundwa kamati maalumu, ofisi za biashara na tume za pamoja za kufufua na kustawisha zaidi biashara.
Uwezeshaji wa soko la mpakani, upanuzi wa vituo vya biashara vya kuvuka mpaka, na kuanzishwa maeneo ya viwanda vya pamoja ni masuala mengine yaliyosisitizwa kwenye kikao cha kamati hiyo.
Mwanzoni mwa mwezi huu kulifikiwa makubaliano ya pande tatu yaliyozihusisha Iran, Pakistan, na Uturuki, chini ya mwamvuli wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi (ECO), kwa ajili ya kufufua huduma za kila mwezi za usafirishaji wa mizigo kwenye ukanda wa reli ya Istanbul-Tehran-Islamabad.