Rais wa Afrika Kusini atoa mwito wa kuwepo taifa huru la Palestina
Wakati vita vya Israel dhidi ya Gaza vikiendelea, Rais wa Afrika Kusini amesisitiza kuhusu dhamira ya nchi yake ya kupatikana njia ya ufumbuzi wa mataifa mawili ili kuhitimisha mzozo uliodumu kwa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amebainisha haya katika hotuba yake kwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kuasisiwa kwa taifa huru la Palestina. Mkutano huo umefanyika chini ya uwenyekiti wa Ufaransa na Saudi Arabia.
Ramaphosa amesema: Afrika Kusini inasisitiza dhamira yake thabiti ya kuundwa kwa taifa lenye mshikamano la Palestina litakoishi kwa amani na taifa la Israel kwenye mipaka ya 1967, na Baitul Muqaddas Mashariki ukiwa mji wake mkuu.
Ameongeza kuwa Israel imetoa adhabu isiyo na uwiano kwa wananchi wa Palestina, na akasema kuasisiwa nchi huru ya Palestina ni njia pekee ya utatuzi wa kadhia ya Palestina.
Rais wa Afrika Kusini pia amezipongeza nchi zote duniani ambazo hivi karibuni zimetangaza kuitambua rasmi Palestina.
Katika Mkutano huo wa Baraza Kuu la UN, Ufaransa, Monaco, Luxemborg na Malta pia zimefuata mkondo huo wa kulitambua rasmi taifa la Palestina.
Nchi hizo zimechukua hatua hiyo baada ya Uingereza, Canada, Australia na Ureno kutangaza kulitambua rasmi taifa la Palestina.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa vizuizi vyote katika kuasisi mataifa mawili vinapasa kuondolewa ikiwa ni pamoja na kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuondolewa kwa ukuta wa kibaguzi.
Israel na Marekani zilisusia mkutano huo kuhusu kuasisiwa kwa ktaifa huru la Palestina.