AU yaisimamishia uanachama Madagascar kufuatia mapinduzi ya kijeshi
Umoja wa Afrika umetengaza kuisimamishia unachama Madagascar "hadi utaratibu wa kikatiba utakaporejeshwa" baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Andry Rajoelina.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na AU imesema kuwa, jumuiya hiyo ya kibara itawawekea watu makhsusi vikwazo iwapo utawala wa kiraia hautarejeshwa nchini humo. Huko nyuma pia, jumuiya hiyo ilisimamishia nchi kadhaa uanachama baada ya mapinduzi ya kijeshi, zikiwemo Mali, Burkina Faso na Guinea.
Siku ya Jumanne, kitengo kile kile cha kijeshi kilichosaidia kuinuka kwa Rajoelina na kuingia madarakani kwa muhula wa kwanza akiwa na miaka 34, kilitangaza kuchukua madaraka nchini Madagascar na kumuondoa madarakani kama rais kufuatia wiki kadhaa za maandamano yaliyoongozwa na vijana - mara hii dhidi ya Rajoelina na serikali yake.
Wakati huo huo, Kanali Michael Randrianirina anatazamiwa kuapishwa kama Rais wa Madagascar kesho tarehe 17 Oktoba, watawala wa kijeshi wa nchi hiyo wamesema katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii na kituo cha televisheni cha serikali.
Mahakama ya Juu ya Katiba ya Madagascar juzi Jumanne "ilimwita" kamanda wa Kituo cha Uendeshaji cha Wafanyakazi wa Jeshi (CAPSAT) Kanali Michael Randrianirina "akatekeleze kazi za mkuu wa nchi."
Ilimtaka Randrianirina aitishe uchaguzi ndani ya siku 60 kwa mujibu wa siku atakayoamua, ikinukuu Kifungu cha 53 cha Katiba, ambacho kinahitaji uchaguzi wa urais ufanyike ndani ya siku 30 hadi 60 baada ya Mahakama Kuu ya Katiba kutangaza kuwa ofisi hiyo imebaki tupu.
Tangu Septemba 25, Rajoelina amekabiliwa na maandamano yanayoongozwa na vijana wa kizazi cha Gen-Z wanaolalamikia uhaba mkubwa wa maji na umeme, pamoja na madai ya rushwa; maandamano ambayo yameenea haraka kote nchini na kugeuka kuwa mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu.