Olmert akiri: Maangamizi ya kizazi cha Wapalestina yanafanyika Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i136326-olmert_akiri_maangamizi_ya_kizazi_cha_wapalestina_yanafanyika_ukingo_wa_magharibi
Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa kizayuni wa Israel Ehud Olmert amekiri kwamba polisi, jeshi na Shirika la Usalama wa Ndani la utawala huo (Shabak) wanahusika katika mashambulizi yaliyopangwa na walowezi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, akielezea vitendo hivyo kama njama ya kijinai na utumiaji nguvu ya uangamizaji wa kizazi cha Wapalestina.
(last modified 2026-02-15T05:39:07+00:00 )
Feb 06, 2026 10:10 UTC
  • Olmert akiri: Maangamizi ya kizazi cha Wapalestina yanafanyika Ukingo wa Magharibi

Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa kizayuni wa Israel Ehud Olmert amekiri kwamba polisi, jeshi na Shirika la Usalama wa Ndani la utawala huo (Shabak) wanahusika katika mashambulizi yaliyopangwa na walowezi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, akielezea vitendo hivyo kama njama ya kijinai na utumiaji nguvu ya uangamizaji wa kizazi cha Wapalestina.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel, Olmert amefichua hali kadhaa za jinai zinazoendelea kufanywa na kusisitiza kwamba makundi ya walowezi wenye silaha na wenye misimamo mikali ya chuki yanawatesa na kuwanyanyasa Wapalestina wanaoishi katika maeneo hayo, ambapo katika matukio mengine hupelekea kujeruhiwa au hata kuuawa Wapalestina hao.

Waziri mkuu huyo wa zamani wa utawala ghasibu wa Israel amefafanua kuhusu mashambulizi hayo akisema, vitendo hivyo vya jinai vinavyofanywa na walowezi ni pamoja na kuchoma moto mashamba ya mizeituni, nyumba na magari, kuvamia faragha za nyumba za Wapalestina na kuwasababishia madhara ya kimwili Wapalestina hao wa Ukingo wa Magharibi.

Olmert amebainisha pia kwamba, washambuliaji hao wanayahujumu hata maisha ya Wapalestina, kwa kushambulia mifugo yao ya kondoo, kuitawanya au kuwaibia.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hapo kabla afisa mmoja wa Palestina, naye pia aliashiria kushadidi kwa mashambulizi ya walowezi wa kizayuni wanaobeba silaha dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu, na akabainisha kwamba, hujuma hizo ni sehemu ya sera inayotekelezwa na utawala wa Kizayuni ya kuutenga Ukingo wa Magharibi, lengo likiwa ni kuvizingira vijiji vya eneo hilo kijiografia na kufungua njia ya kuyavamia na kuyakalia kwa mabavu maeneo zaidi ya Wapalestina.

Nasir Abu Thabit, mkurugenzi wa ufuatiliaji ujenzi wa vitongoji amesema: "mashambulizi yanayoongezeka ya walowezi wa kizayuni katika Ukingo wa Magharibi na Quds inayokaliwa kwa mabavu, ambayo yanafanywa kwa usaidizi na uungaji mkono wa moja kwa moja wa jeshi la Israel, yanaonyesha kuwa vitendo hivi si mashambulizi ya hapa na pale au yanafanywa na mtu binafsi, bali ni sehemu ya sera inayolenga kulazimisha ukweli mpya na kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina katika ardhi zao".../