Mradi wa Mauaji ya Kimbari wa Italia nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136336-mradi_wa_mauaji_ya_kimbari_wa_italia_nchini_libya
Karne ya ishirini Miladia haikushuhudia tu matukio ya kushangaza ya binadamu, bali pia ilibeba baadhi ya kurasa zenye giza kuu katika historia ya mwanadamu. Katika moyo wa bara la Afrika, nchini Libya, dola moja ya kikoloni kutoka Ulaya ilitekeleza mpango wa kishetani na uliopangwa kwa umakini kwa lengo la kuangamiza taifa zima.
(last modified 2026-02-07T05:04:08+00:00 )
Feb 07, 2026 02:37 UTC
  • Mradi wa Mauaji ya Kimbari wa Italia nchini Libya

Karne ya ishirini Miladia haikushuhudia tu matukio ya kushangaza ya binadamu, bali pia ilibeba baadhi ya kurasa zenye giza kuu katika historia ya mwanadamu. Katika moyo wa bara la Afrika, nchini Libya, dola moja ya kikoloni kutoka Ulaya ilitekeleza mpango wa kishetani na uliopangwa kwa umakini kwa lengo la kuangamiza taifa zima.

Ulikuwa ni uhalifu uliowapeleka makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia na ni uhalifu ulioshambulia ustaarabu wa kale, na kuacha jeraha kubwa katika dhamiri ya ubinadamu. Tukio la “Shar” au mauaji ya kimbari ya Libya si janga la eneo moja tu, bali ni alama iliyo wazi ya sura halisi ya ukoloni; sura inayojisitiri nyuma ya kauli mbiu za ustaarabu na maendeleo, huku ikipanda mbegu za uharibifu na maangamizi.

Mauaji ya kimbari ya Libya, ambayo katika kumbukumbu ya pamoja ya watu wa ardhi hii yanajulikana kwa jina la “Shar”, yanaashiria mojawapo ya maafa yaliyo giza na yaliyoandaliwa kwa mfumo madhubuti zaidi katika zama za ukoloni wa karne ya ishirini.

Msiba huu mkubwa ulifikia kilele chake hususan baada ya Vita vya Pili vya Italia na Harakati ya Senoussi, kati ya miaka 1929 hadi 1934, ambapo muundo wa kijamii, kiuchumi na kibinadamu wa mashariki ya Libya, ijulikanayo kama Barqa (Cyrenaica), karibu uliangamizwa kabisa.

Sababu za kutokea kwa janga hili zinapaswa kutafutwa katika mkutano wa itikadi ya kifashisti, mashindano ya kibeberu, na ndoto ya kufufua Dola ya Roma.

Italia, iliyochelewa kuingia katika uwanja wa ukoloni ikilinganishwa na madola mengine ya Ulaya, ilipoivamia Libya mwaka 1911, ilikuwa ikilenga kuunda “Italia Kubwa” na kuimarisha nafasi yake kama dola ya kifalme. Benito Mussolini, kiongozi wa kifashisti wa Italia, aliita Libya “pwani ya nne” ya Italia, na aliiona kuwa ni ardhi iliyopaswa kugeuzwa kuwa ya Kiitalia kikamilifu. Ndoto hii, hata hivyo, iligongana vikali na uhalisia wa kuwepo kwa wakazi wa asili Waarabu na Waberber katika ardhi hiyo.

Upinzani mkali na wa muda mrefu wa wananchi, uliokuwa chini ya uongozi wa harakati ya Senusi na shujaa wao wa kihistoria, Sayyid ‘Umar al-Mukhtar, ulikuwa kikwazo kigumu mbele ya mipango ya upanuzi ya Roma. Hatimaye, viongozi wa kijeshi na kisiasa wa Italia walifikia hitimisho kwamba ili kutimiza ndoto yao ya kikoloni, ilikuwa lazima waangamize kabisa wakazi wa asili.

Barua za makamanda wakuu kama Marshal Pietro Badoglio kwa Jenerali Rodolfo Graziani zinaonyesha wazi nia hii ovu, pale waliposema kwa uwazi juu ya umuhimu wa kuangamiza watu waliotawaliwa. Mtazamo huu, ukiambatana na ubaguzi wa rangi uliopangwa na dharau iliyowaona Waarabu na Waberber kama watu washenzi, uliunda mazingira ya kifikra na kisiasa kwa uhalifu wa kiwango cha mauaji ya kimbari.

Utekelezaji wa mpango huu mchafu ulifuatwa kwa umakini wa kichaa na kwa ukatili wa kimfumo. Moyo wa mauaji haya ya kimbari unaweza kuonekana katika kuanzishwa kwa mtandao mpana wa kambi za kazi ya kulazimishwa. Nyaraka za kihistoria zinaonyesha kuwepo kwa angalau kambi kuu kumi na sita, ambamo takribani watu elfu themanini hadi laki moja wa Barqa, karibu nusu ya wakazi wote wa eneo hilo, walifungwa. Lengo lilikuwa kukata uhusiano kati ya wapiganaji wa Senusi na msingi wao wa kijamii, na kubomoa misingi ya maisha ya kijamii na ya kifugaji.

Hali katika kambi hizi, ambapo kambi ya Swani al-Tariyya ni miongoni mwa chache zenye kumbukumbu zilizosalia, ilibuniwa kwa makusudi kuwa kinyume na utu wa kibinadamu: njaa kali, maradhi ya kuambukiza kama vile taifodi na kifua kikuu, uhaba mkubwa wa maji na dawa, pamoja na msongamano uliosababisha vifo vya halaiki. Maelfu ya watu, wakiwemo wanawake, watoto na wazee, walikufa katika maeneo haya ya mauti. Kilele cha kutisha cha uhalifu huu kilikuwa kunyongwa kwa ‘Umar al-Mukhtār katika kambi ya Suluq mnamo Septemba 1931, mbele ya macho ya wafungwa raia wasiopungua elfu ishirini, ili kutuma ujumbe wa hofu na kusalimu amri kwa watu wote wa Barqa.

Omar Mukhtar, mpigania ukombozi wa Libya kabla ya kuuawa na jeshi katili la kigaidi la Italia

Lakini haya hayakuwa mwisho wa mkasa. Kabla hata ya kuwasili kambini, wengi walikumbana na mojawapo ya sura za kutisha zaidi za sera hii: misafara ya mauti. Makumi ya maelfu ya wakazi wa maeneo yenye rutuba ya Jabal al-Akhdar (Milima ya Kijani), kwa lengo la kuwapa makazi wahamiaji Waitalia, walifukuzwa kwa nguvu kutoka maeneo yao na kulazimishwa kusafirishwa kuelekea majangwa yenye joto kali au vituo vya makazi ya muda. Katika safari hizi za kulazimishwa, zilizoambatana na vipigo na kunyongwa kwa waliopinga, watu wengi walikufa kwa njaa, kiu na uchovu.

Wakati huohuo, jeshi la Italia lilitekeleza uharibifu wa makusudi rasilimali za wananchi. Kuchinjwa kwa mifugo kwa wingi, ambayo ilikuwa uti wa mgongo wa uchumi wa kifugaji, kulifanywa kwa mpangilio maalumu. Takwimu zinaonyesha kuporomoka idadi ya mifugo kwa kiwango cha kutisha: idadi ya kondoo na mbuzi ilishuka kutoka vichwa 126,000 mwaka 1910 hadi 22,000 mwaka 1933, na idadi ya ngamia kutoka 83,000 hadi takribani 2,600. Aidha, ili kuwanyima wapiganaji na raia maji, visima vilizibwa au kutiwa sumu. Zaidi ya hayo, jeshi la Italia lilirekodi mojawapo ya matumizi ya awali na mapana ya silaha za kemikali dhidi ya raia baada ya Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia, kwa kutumia gesi ya haradali dhidi ya maeneo ya makazi na wapiganaji.

Makadirio sahihi ya idadi ya waliouawa katika mauaji haya ya kimbari yamekuwa magumu kutokana na jitihada za mamlaka ya Italia kufuta nyaraka na kuzima habari. Hata hivyo, takwimu zilizopo zinajieleza zenyewe. Idadi ya watu wa Barqa ilishuka kutoka takribani 225,000 mwanzoni mwa operesheni mwaka 1929 hadi 142,000 mwishoni mwake, hali inayoonyesha kuangamizwa kwa karibu theluthi moja ya wakazi. Makadirio ya jumla ya waliouawa katika kipindi hiki yanaanzia watu 20,000 hadi 100,000, na imeripotiwa kuwa katika miaka ya 1930 na 1931 pekee, watu wapatao 12,000 waliuawa kwa madai ya uasi. Umoja wa Mataifa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ulikadiria kuwa katika kipindi chote cha ukoloni wa Italia nchini Libya (1912–1942), kati ya Walibya 250,000 hadi 300,000 walipoteza maisha kutokana na sababu zisizo za kawaida zinazohusiana na vita, ukandamizaji, njaa na magonjwa.

Mauaji haya ya kimbari hayakuijeruhi Libya pekee, bali pia yaliunganika kihistoria na maafa yaliyofuata barani Ulaya. Ziara rasmi za maafisa wakuu wa Nazi, akiwemo Heinrich Himmler na Hermann Göring, nchini Libya katika miaka ya 1938 na 1939 kwa lengo la kushuhudia matokeo ya sera za utakaso wa kikabila na makazi ya kulazimishwa, zinaonyesha kuwa uhalifu katika makoloni ya Afrika wakati mwingine ulifanya kazi kama maabara ya maafa.

Uangamizi uliopangwa wa Libya na utawala wa kikoloni wa Italia haukuwa tu uvamizi wa ardhi, bali ulikuwa ni jitihada ya kufuta kabisa utambulisho wa taifa.

Hata hivyo, upinzani thabiti wa Walibya dhidi ya mradi huu wa mauaji ya kimbari, pamoja na gharama kubwa na za kutisha, ulithibitisha kuwa irada ya taifa haiwezi kufutwa kwa urahisi kutoka katika kurasa za historia.