Kwa nini Trump anaendelea kukariri mkakati ulioshindwa mara nyingi huko nyuma?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139116-kwa_nini_trump_anaendelea_kukariri_mkakati_ulioshindwa_mara_nyingi_huko_nyuma
Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine tena amekiuka makubaliano legevu ya kusitisha mapigano kati ya nchi hiyo na Iran kwa kushambulia upya maeneo kadhaa ndani ya ardhi ya Iran, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya kiraia, hii ikiwa ni siku chache tu baada ya kudai kuwa makubaliano na Iran yalikuwa yanakaribia.
(last modified 2026-06-13T11:03:27+00:00 )
Jun 13, 2026 10:59 UTC
  • Kwa nini Trump anaendelea kukariri mkakati ulioshindwa mara nyingi huko nyuma?

Rais Donald Trump wa Marekani kwa mara nyingine tena amekiuka makubaliano legevu ya kusitisha mapigano kati ya nchi hiyo na Iran kwa kushambulia upya maeneo kadhaa ndani ya ardhi ya Iran, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya kiraia, hii ikiwa ni siku chache tu baada ya kudai kuwa makubaliano na Iran yalikuwa yanakaribia.

Jibu la Iran pia lilikuwa la haraka na la moja kwa moja, huku kambi za kijeshi za Marekani huko Bahrain, Kuwait na Jordan zikilengwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani.

Mzunguko huu unaojirudiarudia unaibua swali la msingi: Je, kwa nini Trump anaendelea kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran licha ya kushindwa mara kwa mara katika uwanja huo? Bila shaka jibu la swali hili linapatikana katika mchanganyiko wa mahesabu ya kisiasa, fikra binafsi za Trump, na mapungufu ya kimuundo ya nguvu za Marekani. Kabla ya kuchukulia siasa za kigeni kuwa uwanja wa onyesho la usimamizi mgumu wa kijiopolitiki, Trump anazichukulia kuwa onyesho la nguvu dhidi ya mahasimu wake. Kwa mtazamo wake, kila mgogoro lazima umalizike kwa mshindi na mshindwa. Mtazamo huu, unaotokana na uzoefu wake wa kibiashara na masuala binafsi, umemfanya ayaone mashinikizo ya kijeshi kama njia bora zaidi ya kuwatwisha wapinzani matakwa yake ya kisiasa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata hivyo, imeonyesha mara chungu nzima katika miongo minne iliyopita kwamba haitasalimu amri mbele ya mashinikizo yoyote kutoka nje. Siku arubaini za vita na zaidi ya miezi mitatu ya usitishaji vita hafifu zimekuwa na matokeo sawa na yale yaliyoonekana katika miaka iliyopita ya siasa za "mashinikizo ya juu zaidi" dhidi yake. Mashambulizi ya kijeshi, mbali na kushindwa kuilazimisha Iran ilegeze misimamo, pia yameimarisha umoja wa ndani, mshikamano wa kijamii na nia ya kisiasa ya mapambano. Hotuba ya Amir Saeed Iravani, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, inathibitisha wazi ukweli huu. Kwamba Iran haikubali kufanya mazungumzo chini ya mashinikizo na haioni vitisho vya kijeshi kama sababu ya kubadilisha mahesabu yake. Katika mtazamo wa kimkakati pia, Trump anakabiliwa na mgongano wa kimsingi. Anataka kuilazimisha Iran ikubali mapatano ya kisiasa kwa kutumia nguvu za kijeshi, lakini shambulio lolote la kijeshi linaharibu nafasi ya kisiasa inayohitajika kwa ajili ya kufikia makubaliano hayo. Uzoefu wa miaka ya hivi karibuni umeonyesha kuwa kila linapofunguliwa dirisha la diplomasia, hatua za kijeshi za Marekani au utawala wa Kizayuni huzuia kufikiwa makubaliano katika uwanja huo. Ni kwa sababu hii, ndio maana wachambuzi wengi wakaamini kuwa kikwazo kikubwa zaidi cha kufikiwa makubaliano si misimamo ya Tehran bali ni kuyumbayumba kwa maamuzi huko Washington.

Sababu nyingine ya kukaririwa siasa zilizofeli za kutumia mabavu dhidi ya Iran inarejea kwenye mapungufu halisi ya nguvu za Marekani. Washington inasalia kuwa nguvu kubwa zaidi ya kijeshi duniani, lakini nguvu ya kijeshi haina maana ya uwezo wa kulazimisha matokeo ya kisiasa. Vita vya Afghanistan, Iraq, na sasa makabiliano na Iran kwa mara nyingine tena yamethibitisha wazi ukweli huu. Marekani inaweza kulipua kwa mabomu baadhi ya maeneo, lakini hilo halimaanishi kuwa inaweza kuharibu nia ya kisiasa ya nchi. Hasa kuhusiana na Iran, ambayo imebuni mifumo mbalimbali ya kuzuia hujuma ya adui tangu miongo kadhaa iliyopita na imeweza kuutwisha upande wa pili gharama kubwa ya kuanzisha migogoro ya aina yoyote.

Wakati huo huo, nafasi ya kijiopolitiki ya Iran pia ni muhimu sana. Lango Bahari la Hormuz linasalia kuwa mojawapo ya njia muhimu zaidi za uchukuzi wa nishati duniani. Kuongezeka mvutano wowote katika eneo hili kunaweza kuathiri mara moja masoko ya kimataifa ya nishati, uchumi wa kimataifa, na hata hali ya kisiasa ya serikali ya Marekani. Ndio maana wataalamu wengi wa Marekani wanaonya kwamba hatua yoyote mpya ya kijeshi dhidi ya Iran inaweza kuongeza pakubwa bei ya nishati na hivyo kuongeza mashinikizo ya kiuchumi kwa raia wa Marekani. Kwa upande mwingine, mashambulizi ya mara kwa mara ya kijeshi ya Marekai pia yameharibu sifa ya kimataifa ya nchi hiyo. Wakati Washington inazungumzia mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria, yenyewe inakosolewa vikali kwa kukiuka usitishaji mapigano na kushambulia miundombinu ya kiraia. Mkanganyiko huu umeongeza pengo kati ya madai ya kimaadili ya Marekani na tabia yake ya kivitendo na hivyo kudhoofisha baadhi ya nguvu zake laini.

Pamoja na hayo, lakini Trump anaendelea kukariri mbinu hiyo kwa sababu njia nyingine mbadala zinamgharimu kisiasa. Kukubali ukweli kwamba mashinikizo ya kijeshi hayawezi kubadilisha misimamo ya Iran kutamaanisha kukubali kushindwa kwa moja ya nguzo zake muhimu za kisiasa. Kwa hivyo, badala ya kurekebisha siasa hizo, White House wakati mwingine inajaribu kukariri siasa hizo hizo kwa nguvu zaidi; mbinu inayoitwa katika fasihi ya kimkakati "kushadidisha mashinikizo kwa ajili ya kufidia kufeli." Lakini tatizo kuu hapa ni kwamba mazingira ya kimkakati ya kanda leo ni tofauti na siku za nyuma. Baada ya vita vya karibuni, Iran sio tu inaendelea kudumisha nguvu yake ya kuzuia hujuma, bali kwa mujibu wa wachunguzi wengi, imevuka hatua ya kujilinda tu na sasa imeingia katika hatua ya ubunifu zaidi wa kudhibiti migogoro.

Katika hali kama hiyo, kila shambulio jipya la Marekani si tu halitapelekea Tehran kubadilisha msimamo bali litaandamana na ongezeko kubwa la gharama kwa Washington. Kwa hiyo, swali la msingi hapa sio kwa nini Iran haisalimu amri, bali kwa nini Trump anaendelea kutekeleza mkakati ambao ushahidi wa nyanjani, uzoefu wa kihistoria, na hata baadhi ya wasomi wa siasa wa Marekani wanaona kuwa umefeli? Madamu jibu la swali hili halitatolewa wazi, mzunguko wa mashambulizi na majibu ya kulipiza kisasi utashadidi na hivyo kuendeleza mgogoro uliopo. Mzunguko ambao, badala ya kuwa ishara ya nguvu, unaonyesha mkwamo wa kimkakati wa Marekani katika kukabiliana na Iran.