Hatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Adui akikosea, atazabwa kibao kikali
-
Sayyid Ahmad Khatami
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema: "Adui wa taifa haelewi lugha ya mazungumzo wala lugha ya kusitisha mapigano, bali anaelewa lugha ya mabavu, ambayo majeshi yetu yamemfanya aielewe vizuri sana na yataendelea kumfanya adui ielewe vizuri zaidi."
Ayatullah Ahmad Khatami amesema: "Suala la kulipiza kisasi lililotokea wiki iliyopita, hasa kuingia Iran katika uwanja wa kuiunga mkono Hizbullah ya Lebanon na kurudi nyuma kwa adui Mzayuni, limetoa jumbe kadhaa muhimu."
Imam wa Swala ya Ijumaa Tehran amesema: "Ujumbe wa kwanza ni kwamba kile maafisa wa jeshi la Iran wanachosema si kauli mbiu tupu, bali wamekitekeleza katika uwanja wa vita. Walitangaza kwamba watajibu iwapo kutafanyika uchokozi wowote dhidi ya vitongoji vya kusini mwa Beirut, na wametimiza ahadi yao kwa vitendo."
Amesisitiza kuwa: "Leo pia, utawala wa Kiislamu nchini Iran si wa kauli mbiu tu na unawatangazia maadui zake kwamba hatua yoyote ya uchokozi itakabiliwa na jibu kali na la uhakika."
Khatami amesema: "Ujumbe wa pili wa matukio haya ni kwamba watu wa Iran wanakabiliwa na maadui wanaovunja ahadi na mikataba yao; maadui ambao hawazingatii ahadi zao na wana historia ya uchokozi na uvunjaji wa ahadi."
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameongeza: "Adui haelewi lugha ya mazungumzo na kusitisha mapigano na anarudi nyuma tu anapowajihiana na nguvu na mabavu."
Ayatullah Khatami amesema: "Mchango uliotolewa na Ansarullah wa Yemen, Hizbullah ya Lebanon na Vikosi vya Uhamasishaji vya Wananchi wa Iraq katika uwanja huu ni dhihirisho la mshikamano na umoja miongoni mwa harakati za Muqawama."
Ameongeza kuwa: "Taifa la Iran linajiona katika mstari wa mbele wa kutetea maadili, utu na thamani ambazo zina mizizi katika utamaduni wa Ashura na harakati ya mapambano ya Imam Hussein bin Ali (AS).
Sayyid Ahmad Khatami ameendelea na hotuba yake kwa kusema: "Kauli mbiu ya mapambano ya Ashura ya Imam Hussein ya kupinga dhulma na uonevu iko hai katika maisha ya taifa la Iran, na mwaka huu wananchi wameonyesha dhihirisho la kivitendo la kauli mbiu hiyo."
Katika sehemu nyingine ya hotuba zake za Swala ya Ijumaa, Ayatullah Ahmad Khatami amezungumzia dhana ya kumtumainia Mungu na kusema: "Mwanadamu anapaswa kuwa na tumaini na Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye peke yake katika mambo yote. Hakika ya kutawakali ni wakati mwanadamu anapomwamini Mungu kwa vitendo na kumuona Yeye kama chanzo kikuu cha mambo yote."
Ameongeza kwa kusema: "Ni jambo zuri kwa mwanadamu kuzungumzia tawakuli na kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa maneno, lakini ni muhimu zaidi kumtambua Mungu kuwa Ndiye Muweza wa kila kitu katika vitendo na kuchukua maamuzi na kutenda kwa mujibu wa imani hiyo."