Iran yaonya: Mashambulizi dhidi ya miundombinu yetu yatajibiwa kikamilifu
-
Mohammad Baqer Zolqadr
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Baqer Zolqadr, ametoa onyo kali na la moja kwa moja katika ujumbe wake kupitia mtandao wa X siku ya Ijumaa, akijibu vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Katika msimamo wake usioyumba kuhusu usalama wa taifa, Zolqadr ametoa tahadhari nzito kwa Marekani na utawala haramu wa Kizayuni.
Amesema: “Kama tulivyotangaza hapo awali, shambulio lolote dhidi ya miundombinu [ya Iran] litajibiwa kwa hatua za kijeshi za aina hiyo hiyo na kwa ukali uleule.”
Ameongeza kuwa utawala utendao jinai wa Israel, ambao ndio unaochezea kamba nyuma ya vitendo hivi vya kichokozi, hauko salama dhidi ya mkono mrefu wa majeshi ya Iran.
Onyo hili linakuja baada ya Trump kutishia kulenga madaraja na vituo vya kuzalisha umeme vya Iran mapema wiki hii. Jeshi la Marekani lilishambulia mikoa kadhaa siku ya Jumatano na Alhamisi, likilenga maeneo ya kijeshi na ya kiraia na kusababisha vifo vya Wairani wasiopungua 14. Mashambulizi haya na vitisho hivyo ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Maelewano (MoU) uliotiwa saini mwezi uliopita kati ya Tehran na Washington kwa ajili ya kusitisha vita. Mashambulizi hayo yalijibiwa mara moja na Iran, ambapo kambi za Marekani katika nchi kadhaa za kanda hii zililengwa na makombora na ndege zisizo na rubani.
Katibu huyo wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa amemtaja Trump kama “mtu anayechukiwa zaidi duniani,” ambaye amethubutu kulihutubu taifa kubwa na lenye huzuni la Iran kwa lugha ambayo “yeye mwenyewe ndiye anayestahili kuambiwa.”
Zolqadr pia amebainisha kuwa Rais wa Marekani amekasirishwa na mwamko mkubwa wa wananchi waliojitokeza kwa wingi nchini Iran na Iraq wakati wa misafara ya kumuaga Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Kwa mujibu wa ripoti, takriban Wairani milioni 43 na wapenzi wa Mapinduzi kutoka kote duniani walishiriki katika mazishi ya marehemu Ayatullah Khamenei kuwa tukio kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani.
Shughuli za kuaga na mazishi ya Kiongozi huyo mtukufu, zilizochukua siku sita, zilifanyika katika miji mitano – Tehran, Qom, Najaf, Karbala, na Mashhad – zikivutia umati mkubwa wa watu wenye mapenzi makubwa, hali ambayo imeweka rekodi isiyoweza kufutika.