Mradi wa reli ya Ankara–Riyadh waibua wasiwasi Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i139120-mradi_wa_reli_ya_ankara_riyadh_waibua_wasiwasi_israel
Pendekezo la kuanzisha ukanda mpya wa biashara na usafirishaji unaoendelezwa na Uturuki na Saudi Arabia limeibua wasiwasi miongoni mwa maafisa wa utawala wa Israel.
(last modified 2026-06-14T03:08:45+00:00 )
Jun 14, 2026 03:02 UTC
  • Mradi wa reli ya Ankara- Riyadh waibua wasiwasi Israel
    Mradi wa reli ya Ankara- Riyadh waibua wasiwasi Israel

Pendekezo la kuanzisha ukanda mpya wa biashara na usafirishaji unaoendelezwa na Uturuki na Saudi Arabia limeibua wasiwasi miongoni mwa maafisa wa utawala wa Israel.

Wakuu wa utawala wa Kizayuni wanautazama mradi huo kama kama changamoto inayoweza kujitokeza dhidi ya miradi ya miunganisho ya kikanda inayoungwa mkono na utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Jumanne, Uturuki na Saudi Arabia zilisaini hati mbili za makubaliano (MoU) za kupanua ushirikiano katika sekta ya lojistiki na reli, huku mataifa hayo mawili yakichunguza uwezekano wa kuanzisha njia mpya za ardhini zitakazounganisha Ghuba ya Uajemi na Uturuki pamoja na bara la Ulaya.

Hadi sasa, Uturuki Saudi Arabia hazijatangaza hadharani maelezo ya mwisho ya mradi huo unaoripotiwa wa ukanda wa usafirishaji.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Jumamosi na gazeti la Kizayuni  la Yedioth Ahronoth, njia hiyo ya nchi kavu inayopendekezwa intaunganisha mataifa ya Ghuba ya Uajemi na Ulaya kupitia Syria na Jordan kabla ya kuingia Uturuki, hivyo kupita mbali na maeneo yanayokaliwa na Israel na kupunguza utegemezi wa miundombinu ya Israel, ikiwemo bandari ya Haifa.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa ukanda huo unaweza kujitokeza kama mshindani wa Mradi wa Kiuchumi wa India–Mashariki ya Kati–Ulaya (IMEC), ambao ni mpango mkubwa wa biashara unaoungwa mkono na Israel, Marekani, India na baadhi ya mataifa ya Kiarabu.

IMEC imekuwa ikitangazwa kama njia ya kimkakati inayolenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Asia na Ulaya kupitia maeneo yanayodhibitiwa na utawala wa Israel.

Kwa mujibu wa maafisa wa Israel walionukuliwa na gazeti hilo, mpango wa Uturuki na Saudi Arabia unaonekana kama changamoto ya kijiografia na kiuchumi inayoweza kupunguza nafasi ya Israel kama kitovu cha usafirishaji katika eneo hilo.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa maafisa wa utawala huo wanafuatilia kwa karibu maendeleo hayo, wakihofia kuwa mitandao mbadala ya usafirishaji inaweza kudhoofisha umuhimu wa kimkakati wa IMEC pamoja na miundombinu ya usafirishaji ya Israel.

Maendeleo haya yanajiri huku uhusiano kati ya Uturuku na Israel ukizidi kudorora, ambapo Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamebadilishana kauli kali hadharani katika siku za karibuni.

Mabadilishano hayo ya kauli kali yanaakisi kuzorota zaidi kwa uhusiano kati ya Uturuki na Israel tangu kuanza kwa vita vya kikanda vinavyohusisha Gaza, Lebanon, Syria na Iran.

Uturuki, ambayo ni mwanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO, imedai kuwa imesitisha biashara na Israel na imejitokeza kama mmoja wa wakosoaji wakubwa wa utawala huo katika jukwaa la kimataifa.