Muungano wa upinzani DRC wasisitiza msimamo wa mazungumzo jumuuishi ya kitaifa
-
Wapinzani DRC
Muungano wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unaojulikana kama C64 (Coalition Article 64), umesisitiza msimamo wake wa kumtaka Rais Félix Tshisekedi kuitisha mazungumzo ya kitaifa yanayowahusisha watu wote kabla ya tarehe 15 Agosti 2026, au wachukue hatua za kisiasa.
Muungano huo wa upinzani unatishia kuitisha maandamano huku uamuzi wake wa Agosti 15 kwa Rais Félix Tshisekedi ukikaribia tarehe yake ya mwisho ya kuitisha rasmi mazungumzo ya kitaifa jumuishi yanayokusudiwa kutatua mgogoro wa kisiasa na usalama nchini humo.
Upinzani hapo awali ulitangaza maandamano makubwa kisha ukayaahirisha kwa ombi la viongozi wa kidini wanaoyofanya kazi kama wapatanishi na rais Tshisekedi.
Muungano wa C64 ulitangaza tarehe 15 Agosti 2026 yaani kesho Jumamosi kuwa siku ya mwisho ya rais kutangaza rasmi mazungumzo hayo.
Hapo awali, upinzani uliahirisha maandamano yao mjini Kinshasa kufuatia upatanishi wa viongozi wa dini (CENCO na ECC) ili kutoa nafasi kwa mchakato wa mazungumzo.
Serikali ya Jamhuuri ya Kidemokrasia ya Congo imekataa kushinikizwa na kueleza kuwa ratiba ya rais haiongozwi na vitisho vya makataa kutoka kwa wanasiasa.
Viongozi wakuu wa upinzani wamepanga kukutana kesho tarehe 15 Agosti kupanga mikakati mipya endapo tarehe hiyo itapita bila utekelezaji wowote wa kuitishwa mazunguumzo hayo ya kitaifa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, wanasiasa wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ambao ni wanachama wa muungano wa upinzani wa "C64", wamepinga vikali uamuzi wa Mahakama ya Katiba kuhusu sheria ya kura ya maoni, ambayo inaweza kumfungulia njia Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi kugombea urais kwa muhula wa tatu baada ya kura hiyo ya maoni.