Hizbullah: Tuna imani Iran itailinda Lebanon katika makubaliano yoyote na Marekani
-
Hassan Fadlallah
Makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani yatakuwa na matokeo ya moja kwa moja kwa Lebanon bila kujali kuwa mamlaka za Lebanon zinakubali au la.
Hayo yamesemwa mbunge wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kudai kuwa makubaliano na Tehran yanakaribia.
Hassan Fadlallah, Mjumbe wa Kambi ya Uaminifu Kwa Muqawama katika Bunge la Lebanon amesema Iran imetilia mkazo kuijumuisha Lebanon katika mapatano yoyote itakayofikia na Washington.
Fadlallah amesisitiza kuwa hii haimaanishi kuwa Tehran inataka kufanya maamuzi kwa ajili ya Lebanon, bali inataka serikali ya Beirut ifaidike na mapatano hayo.
"Iran imesimama na Lebanon, na inapinga makubaliano yoyote ambayo hayajumuishi kusitishwa mashambulizi dhidi ya Lebanon," ameeleza Fadlallah. Wakati huo huo apuuza madai kwamba vita vya Muqawama dhidi ya Israel vinatumikia maslahi ya Iran na kuyataja madai hayo kuwa "uongo usio wenye lengo la kuficha ukweli."
Mjumbe huyo wa Kambi ya Uaminifu Kwa Muqawama katika Bunge la Lebanon pia amewakosoa viongozi wa nchi hiyo kwa kukiuka ahadi yao ya kutoshiriki mazungumzo na Israel kabla ya kufikiwa usitishaji vita; akiitaja hatua hiyo kuwa ni kudharau damu za mashahidi.
"Tunawezaje kuketi meza moja na wale wanaoendeleza uhalifu wao dhidi ya watu wa Lebanon, huku adui akijivunia ushiriki wa Marekani katika mradi wake wa uharibifu dhidi ya Lebanon, na serikali ya Lebanoni inasalia kimya mbele ya jinai hizo? Amehoji Hassan Fadlallah.
Faili la Lebanon limekuwa nguzo kuu katika mazungumzo ya Marekani na Iran. Jumapili iliyopiita, Iran ilifanya mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel kulipiza kisasi shambulio la utawala huo haramu katika vitongoji vya kusini mwa Beirut.