Tucker Carlson: Marekani imeshindwa kufungua Lango-Bahari la Hormuz
-
Tucker Carlson
Tucker Carlson, mwanahabari maarufu wa kihafidhina wa Marekani, amesema kwamba matukio ya sasa katika mzozo wa Asia Magharibi yanaonyesha mapungufu ya nguvu ya kijeshi ya Marekani, akisisitiza kwamba Washington imeshindwa kufungua tena Lango-Bahari la Hormuz licha ya kutumia gharama kubwa.
Tucker Carlson ametangaza kwenye chaneli yake ya YouTube kwamba: "Hata kwa kuwa na meli za kubeba ndege zenye thamani ya dola bilioni 120, Marekani imeshindwa kulinda Lango-Bahari la Hormuz."
Akiashiria kwamba kuna masuala ambayo Marekani haiwezi kuyatatua kwa urahisi, ameongeza kuwa: Mgogoro wa hivi sasa unaonyesha uwezo mdogo wa Washington; na kupanuka mgogoro wa Asia Magharibi kunaonyesha jinsi viongozi wa Marekani walivyopoteza kikamilifu uwezo wa kuchukua maamuzi muhimu ya sera za kigeni za nchi hii.
Mtangazaji huyo maarufu wa Marekani pia amezungumzia kauli za Trump zinazorudiwarudiwa kuhusu makubaliano tarajiwa ambayo hayatekelezwi, akisisitiza: "Kauli hizi zinazorudiwarudiwa na zisizo na matunda zinatilia shaka ufanisi wa michakato ya mazungumzo."
Awali, gazeti la Guardian lilikuwa limemtaja Rais wa Marekani, Donald Trump, kuwa ni msimuliaji asiyeaminika wa vita dhidi ya Iran, na kuandika kwamba amezungumzia mara kwa mara kuhusu kukaribia kufikiwa makubaliano na Iran, lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa, na badala yake mvutano na mashambulizi ya kijeshi ya pande mbili yameendelea.
Gazeti la Ufaransa la Le Monde pia limeandika katika makala yenye kichwa cha habari "Udhaifu wa Trump katika Mtego wa Iran" kwamba kauli mbiu ya Rais wa Marekani ya "amani kupitia nguvu" haikuwa na tija katika kesi ya Iran.
Chombo hicho cha habari cha Ufaransa kimesisitiza kwamba vita vya Iran vimekuwa na gharama ya kisiasa kwa Trump, na matarajio ya yanayojiri, badala ya kufanana na ushindi wa haraka kwa Washington, yanaelekea kwenye makubaliano ambayo yako mbali na malengo ya awali ya Marekani.