Je, Trump ni rais wa amani kama anavyodai mwenyewe?
-
Donald Trump
Donald Trump, ambaye anajiona kama rais wa amani, amekariri madai yake dhidi ya uwezo wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuhalalisha mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, akidai kwamba bila hivyo, amani katika Asia Magharibi isingewezekana.
Siku ya Jumatano, Februari 4, Trump alirudia madai yake yanayokinzana, akisema: "Kama unavyojua, wao (Iran) wanazungumza nasi" na kudai kuwa: "Kama tusingeharibu uwezo wa nyuklia wa Iran, tusingepata amani katika eneo la Asia Magharibi."
Akiendelea na madai yake, Trump alirudia vitisho vyake, akisema: "Nimesikia kwamba Iran inataka kuanzisha tena mpango mpya. Ikiwa ndivyo ilivyo, tutatuma wanajeshi kufanya hivyo tena [kushambulia vituo vya nyuklia]. Walijaribu kurudi kwenye kituo hicho, lakini hawakuweza kukifikia. Tuligundua kwamba walitaka kuanzisha kituo cha nyuklia katika sehemu nyingine ya nchi. Nimesema, 'Mkifanya hivyo, tutakutendeeni mambo mabaya sana.'"
Trump ametoa Kauli mpya za vitisho dhidi ya Iran wakati ambapo amekuwa akizungumzia diplomasia na kwamba anafadhilisha njia ya kidiplomasia kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika miezi ya hivi karibuni, mjadala kuhusu iwapo Donald Trump kweli ni "Rais wa Amani" kama anavyodai hasa kuhusu Iran, umekuwa mjadala mkali wa kisiasa. Jibu la swali hili linakuwa wazi kwa kuchunguza misimamo yake ya sera za kigeni na mienendo yake kuhusu Iran, na si kusikiliza tu kauli mbiu za Trump na madai yake kwenye vyombo vya habari.
Trump amejionyesha mara kwa mara kama rais anayetaka amani na amekosoa vita vinavyosababisha gharama kubwa za kibinadamu na kifedha; lakini mienendo yake kuhusu Iran, hasa wakati wa muhula wake wa pili, unaonyesha picha tofauti. Katika muhula wake wa pili, Trump amefufua sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran, ambayo ni mchanganyiko wa vikwazo vikubwa na shadidi vya kiuchumi pamoja na vitisho vya kijeshi. Lengo la sera hii si tu kusimamisha miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani nchini Iran, hasa urutubishaji wa urani, lakini pia kuzidisha mashinikizoya kisiasa kwa Tehran ili kutimiza matakwa mengine ya Marekani, ikiwa ni pamoja na kupunguza uwezo wake wa makombora na kubadilisha sera ya kikanda kwa kusitisha misaada kwa makundi ya Muqawama na mapambano ya ukombozi.
Mnamo Juni 2025, Marekani ilifanya mashambulizi ya anga kwenye vituo vitatu muhimu vya nyuklia vya Iran ili kuunga mkono vita vya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Trump amedai mara kwa mara kwamba ameharibu vituo hivyo, kitendo ambacho kilikuwa mojawapo ya hatua kubwa zaidi za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran tangu 1979. Shambulio hilo ni mfano wazi wa matumizi ya nguvu dhidi ya Iran. Tangu wakati huo, Trump ameitishia Iran mara kadhaa kwamba kama Tehran haitatii matakwa ya Washington, kama vile kusimamisha urutubishaji wa urani, ataishambulia Iran. Hata amesema kwamba hataweka kando chaguo la shambulio la haraka la "kasi na kali" ikilazimika, na vitisho hivi vimeambatana kutuma vikosi vya majeshi ya Marekani na zana za kivita katika maeneo ya kandokando ya Iran. Vitisho hivi si tu kwamba vimezidisha mvutano bali pia vimeilazimisha Iran kutoa mijibizo na majibu makali zaidi.
Katika suala hili, wachambuzi wa kisiasa wanaelezea sera ya Trump kuhusu Iran kuwa ni kielelezo cha diplomasia ya "karoti na rungu." Katika suala hili, sambamba na juhudi zinazodaiwa kufanywa na utawala wa Trump za kuzungumza na Iran, uwepo mkubwa wa jeshi na vitisho vya kijeshi vinatumika kama chombo cha shinikizo. Mbinu hii pia inaonekana kuhusiana na utumiaji wa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran katika urais wa Trump, ambayo hutumia mashinikizo ya kiuchumi na kijeshi ili kulazimisha mabadiliko ya msingi katika sera za ndani za Iran.
Kwa hivyo japokuwa Trump anatoa nara za amani, lakini vitendo na mbinu zake kuhusiana na Iran zinaonyesha zaidi ya tishio la chaguo la kijeshi, hasa anapotumia zana za kivita kama wenzo wa kuwa na nafasi nzuri katika meza ya mazungumzo. Kwa hivyo, madai kwamba Trump ni "rais wa amani" tu hayaoani na hali halisi ya sera yake ya kigeni kuhusu Iran, hasa wakati vitisho vyake vya mara kwa mara vya kutumia mabavu na uwepo wake mkubwa wa majeshi ya nchi hiyo vinapounganishwa na madai yake ya kidiplomasia.
Kwa upande mwingine, maafisa wakuu wa kisiasa na usalama wa Iran wamepinga vitisho vya kijeshi na kutangaza kwamba wanaamini kuwa suluhisho la hitilafu linapatikana kwenye meza ya mazungumzo. Tehran imetangaza kwamba iko tayari kuzungumza kwa masharti sawa na ya haki. Tarehe 3 mwezi huu wa Februari, Masoud Pezekian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Kwa kuzingatia ombi la nchi rafiki katika eneo hili kuhusu pendekezo la Rais wa Marekani la kufanya mazungumzo, nimemwagiza Waziri wa Mambo ya Nje kutayarisha uwanja wa mazungumzo ya haki na uadilifu kwa kuuzingatia kanuni za utu, hekima, ndani ya mfumo wa maslahi ya kitaifa, ikiwa kuna mazingira yanayofaa yasiyo na vitisho na mbali na matarajio yasiyo na msingi."