AU, UN zalaani mashambulizi ya kigaidi yaliyoua 170 Nigeria
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na nchi mbali mbali duniani sambamba na kutoa salamu za rambirambi, zimelaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyoua watu wasiopungua 170 magharibi mwa Nigeria.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf ameliita shambulio hilo kuwa "kitendo cha kikatili na cha kinyama," ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na hujuma "isiyokubalika" dhidi ya amani na usalama.
Youssouf amesema Umoja wa Afrika unasisitiza kwa mara nyingine tena kujitolea kwake kuunga mkono juhudi za Nigeria za kuimarisha amani, usalama na utulivu kote nchini.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amelaani shambulio hilo katika Jimbo la Kwara, akitoa rambirambi kwa familia za waathiriwa na serikali ya Nigeria, huku akiwatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa.
Guterres amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na Abuja katika mapambano yake dhidi ya ugaidi na misimamo ya kufurutu ada, akisisitiza umuhimu wa kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.
Kwa mujibu wa mbunge wa jimbo la magharibi la Kwara, Saidu Baba Ahmed, watu wenye silaha waliivamia jamii ya Woro Jumanne jioni, na kuwaua watu wasiopungua 170.
Wakati huohuo, wakazi wa jimbo la Katsina lililoko kaskazini ya Nigeria wamesema, watu wasiopungua 21 waliuawa kwa kupigwa risasi na washambuliaji waliowaandama walengwa kutoka nyumba hadi nyumba.
Mauaji ya huko Kwara ni shambulio baya zaidi kufanyika kwenye eneo hilo katika miezi ya hivi karibuni.