Tanzania, Uganda kuanza kuuza mafuta ghafi Julai mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136382-tanzania_uganda_kuanza_kuuza_mafuta_ghafi_julai_mwaka_huu
Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema mafuta ghafi yatakayopita katika Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania yataanza kusafirishwa kwenda sokoni ifikapo Julai, mwaka huu.
(last modified 2026-02-08T02:48:01+00:00 )
Feb 08, 2026 02:48 UTC
  • Tanzania, Uganda kuanza kuuza mafuta ghafi Julai mwaka huu
    Tanzania, Uganda kuanza kuuza mafuta ghafi Julai mwaka huu

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema mafuta ghafi yatakayopita katika Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania yataanza kusafirishwa kwenda sokoni ifikapo Julai, mwaka huu.

Rais Samia amebainisha hayo jana wakati wa ziara ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na kujadiliana masuala kadhaa ukiwamo mradi wa Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga.

Wakizungumza na vyombo vya habari, viongozi hao wameeleza mambo waliyoyajadili kwenye mazungumzo yao ya faragha na baada ya kukutana na timu zao za mawaziri huku waliangazia masuala mtambuka.

Rais Samia amesema timu za mawaziri na wasaidizi wao zilikutana wakati wao wakifanya mazungumzo ya faragha na kwamba, miongoni mwa mambo waliyojadili ni ujenzi wa mabomba ya nishati.

Mbali na bomba la kusafirisha mafuta ghafi la EACOP, amesema wamejadili pia kuhusu bomba la gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda na bomba la mafuta safi kutoka Uganda kwenda Tanga.

Rais Samia ameongeza kuwa wamejadiliana pia kuhusu bandari kwa kuwa Tanzania inategemewa na nchi ambazo hazina bahari, hivyo wamejadiliana namna watakavyozitumia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Kwa upande wa reli, amesema wamewaeleza wenzao wa Uganda kuhusu mradi wa reli kutoka Tanga hadi Musoma na huko wataweza kuunganisha kwa meli hadi Uganda.

Pia, amesema wamewaeleza kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ya Isaka hadi Rusaunga na kwamba wameiomba Uganda nayo ipokee ujenzi wa reli hiyo hadi Murongo kwa upande wa Uganda.