Mahakama ya Madagascar "yamwita" kanali wa jeshi akachukue uongozi na kuitisha uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132006-mahakama_ya_madagascar_yamwita_kanali_wa_jeshi_akachukue_uongozi_na_kuitisha_uchaguzi
Mahakama ya Juu ya Katiba ya Madagascar jana Jumanne "ilimwita" kamanda wa Kituo cha Uendeshaji cha Wafanyakazi wa Jeshi (CAPSAT) Kanali Michael Randrianirina "akatekeleze kazi za mkuu wa nchi."
(last modified 2025-10-15T09:12:33+00:00 )
Oct 15, 2025 06:02 UTC
  • Mahakama ya Madagascar

Mahakama ya Juu ya Katiba ya Madagascar jana Jumanne "ilimwita" kamanda wa Kituo cha Uendeshaji cha Wafanyakazi wa Jeshi (CAPSAT) Kanali Michael Randrianirina "akatekeleze kazi za mkuu wa nchi."

Katika taarifa yake, mahakama hiyo imeitangaza ofisi ya rais wa nchi hiyo kuwa imebaki "tupu," baada ya viongozi wa CAPSAT, wakiongozwa na Randrianirina, kuingia ikulu ya Ambohitsorohitra katika mji mkuu Antananarivo siku ya Jumanne na kutangaza kwamba wameshika hatamu za madaraka.

Mahakama ya Katiba ya Madagascar imemtaka Randrianirina aitishe uchaguzi ndani ya siku 60 kwa mujibu wa siku atakayoamua, ikinukuu Kifungu cha 53 cha Katiba, ambacho kinahitaji uchaguzi wa urais ufanyike ndani ya siku 30 hadi 60 baada ya Mahakama Kuu ya Katiba kutangaza kuwa ofisi hiyo imebaki tupu.

Imesema Rais Andry Rajoelina hawezi kutimiza wajibu wake kwa sababu "hayupo, na hawezi kuwapo" nchini humo, ikiwa ni sawa na "kutelekeza madaraka bila mpangilio."

Mapema hapo jana, jeshi lilisema urais wa nchi hiyo utachukuliwa na maafisa wake na kwamba kipindi cha mpito kitarefushwa kwa miaka miwili na kitajumuisha kura ya maoni ya uundaji wa katiba mpya.

Taasisi tano za nchi zikiwemo Mahakama ya Juu ya Katiba, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Seneti, Baraza Kuu la Kutetea Haki za Kibinadamu na Mahakama ya Juu ya Haki, zimesimamishwa huku Bunge likiendelea kubaki madarakani.

Mapema jana hiyohiyo, Rajoelina, ambaye ameripotiwa kuwa amekimbilia Ufaransa, alivunja bunge kufuatia wiki kadhaa za maandamano dhidi ya serikali kote nchini, akisema ni muhimu kurejesha utulivu na kutoa nafasi kwa vijana.

Hata hivyo, bunge lilikutana na kupitisha hoja ya kumsaili rais.../