Kimbunga Gezani chaikumba Madagascar, chaua 20 na kujeruhi 33
-
Kimbunga Gezani chaikumba Madagascar, chaua 20 na kujeruhi 33
Kimbunga cha Tropiki cha Gezani kimepiga mji wa bandari wa Toamasina ulioko kwenye pwani ya mashariki mwa Madagascar, na kuua watu wasiopungua 20 na kujeruhi wengine 33 katika jiji hilo la pili kwa ukubwa kwenye kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, huku mvua kali na upepo vikisababisha uharibifu mkubwa. Hayo ni kwa mujibu wa mamlaka husika ya nchi hiyo.
Ofisi ya usimamizi wa maafa ya Madagascar imesema watu 33 wamejeruhiwa na wakazi wasiopungua 1,500 wamehamishwa katika wilaya ya karibu na mji huo baada ya kimbunga kupiga eneo hilo usiku wa kuamkia Jumatano.
Wakazi kadhaa wa maeneo hayo ya Toamasina wameelezea athari ya kimbunga hicho.
"Sijawahi kuhisi upepo mkali kiasi hiki... Milango na madirisha yameharibiwa," amesema Harimanga Ranaivo.
Kwa mujibu wa ofisi ya masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, hicho kilikuwa kimbunga cha pili kuikumba Madagascar mwaka huu, siku 10 baada ya kimbunga cha tropiki Fytia kuua watu 14 na kusababisha zaidi ya watu 31,000 kuhama makazi yao.
Gezani imeambatana pia na upepo mkali uliokuwa na kasi ya karibu kilomita 185 kwa saa, na mawimbi ya upepo yalifikia karibu kilomita 270 kwa saa — huku ukiezua mapaa na kuangusha miti.
Kabla ya kimbunga hicho kuwasili, serikali ilifunga skuli na kuandaa makazi ya dharura.
Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Madagascar awali ilitahadharisha kuongezeka kwa kiwango cha bahari.
Hata hivyo, kufikia Jumatano asubuhi, Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Madagascar ilisema, Kimbunga Gezani kilikuwa kimepungua kasi, na kilikuwa kimeelekea magharibi mwa nchi, takriban kilomita 100 kaskazini ya mji mkuu Antananarivo.
"Gezani itavuka milima ya kati kutoka mashariki hadi magharibi leo, kabla ya kusogea baharini katika Mfereji wa Msumbiji jioni hii au usiku wa leo," ilieleza Mamlaka hiyo.../