Jinai za Marekani nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i132018-jinai_za_marekani_nchini_syria
Marekani imekuwa nchini Syria tangu mwaka 2014 kwa kisingizio cha kupambana na ISIS na imefanya jinai nyingi nchini humo.
(last modified 2025-10-15T08:44:25+00:00 )
Oct 15, 2025 08:44 UTC
  • Jinai za Marekani nchini Syria

Marekani imekuwa nchini Syria tangu mwaka 2014 kwa kisingizio cha kupambana na ISIS na imefanya jinai nyingi nchini humo.

Kwa mujibu wa Pars Today, Marekani iliingia Syria mwaka 2014 kwa kisingizio cha kupambana na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na kuunda muungano uliodaiwa wa kimataifa wa eti kupambana na magaidi hao wa ISIS. Ingawa uvamizi huo wa kijeshi ulifanywa kwa lengo lililodaiwa ni la kupambana na ugaidi, lakini matokeo yake yalikuwa mabaya na ulisababisha mashambulizi ya kijeshi, uharibifu wa miundombinu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Kwa hakika, jinai za Marekani nchini Syria si tu zimesababisha uharibifu mkubwa dhidi ya binadamu na miundombinu, lakini pia zimeleta madhara makubwa ya kijiografia na haki za binadamu kwa eneo hili na dunia nzima kiujumla. Marekani imefanya jinai nyingi za wazi na za siri nchini Syria, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia, uharibifu wa miundombinu, uporaji wa rasilimali na vikwazo vya kiuchumi. Takwimu rasmi kuhusu haki za binadamu zilizovunjwa na Marekani nchini Syria ni pamoja na:

Mosi: Mashambulio makubwa ya mabomu na vifo vya raia

- Maelfu ya raia wa Syria wameuawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Marekani kwenye miji kama vile Raqqa, Deir Ezzor na Hasakah. Mwaka 2017, muungano vamizi unaoongozwa na Marekani ulianzisha operesheni kubwa ya eti kuukomboa mji wa Raqqa kutoka kwa magaidi wa Daesh (ISIS). Makumi ya hospitali, skuli na vituo vya maji katika mikoa ya Raqqa na Deir Ezzor viliharibiwa kwenye mashambulizi ya anga ya Marekani. Umoja wa Mataifa ulisema wakati huo kwamba asilimia 90 ya miundombinu ya mijini ya Raqqa imeharibiwa na mashambulizi ya muungano huo ulioongozwa na Marekanhi. Ripoti rasmi za haki za binadamu zinaonyesha kuwa muungano unaoongozwa na Marekani umefanya uhalifu mkubwa wa kivita huko Raqqa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya silaha zilizopigwa marufuku na kushambulia makazi ya raia. Wengi wa wahanga wa mashambulizi hayo ni watoto wadogo, wanawake na wazee wanaoishi katika maeneo ya raia. Kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch, zaidi ya raia 1,600 waliuawa katika operesheni hiyo, wengi wao wakiuawa katika mashambulizi ya kiholela ya anga yaliyoongozwa na Marekani huko Syria.

Pili: Uharibifu wa miundombinu muhimu

- Mashambulizi ya anga ya Marekani nchini Syria yameharibu mahospitali, maskuli, madaraja na vituo muhimu vya maji katika maeneo yaliyokuwa yanadhibitiwa na Daesh. Uharibifu huo si tu ulilemaza maisha ya watu, lakini pia ulifanya iwe vigumu kwa serikali ya wakati huo ya Syria kuijenga upya nchi baada ya vita. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba jinai hizo zilifanywa kwa makusudi na Marekani kwa lengo la kuidhoofisha serikali ya Rais wa Syria wa wakati huo Bashar al-Assad na hazikulenga kupambana na magaidi wa ISIS.

Lori la mafuta la Marekani likipora mafuta ya Syria mchana kweupe

Tatu: Uporaji wa rasilimali za mafuta ya Syria

- Wanajeshi vamizi wa Marekani walidhibiti visima vya mafuta katika maeneo yenye utajiri wa mafuta mashariki mwa Syria, hasa katika jimbo la Hasakah. Ripoti za kuaminika zinasema kuwa, Marekani, kwa kushirikiana na wanamgambo wa ndani, ilichimba mafuta ya Syria na kuyasafirisha nje ya nchi kwa wizi. Serikali ya wakati huo ya Syria ilifungua mashtaka kwenye taasisi za kimataifa kulalamikia uporaji na wizi huo wa Marekani wa rasilimali za wananchi wa Syria na kusisitiza kwamba huo ulikuwa ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa Syria. Kwa mujibu wa Wizara ya Mafuta ya Syria ya wakati huo, takriban mapipa 80,000 ya mafuta yalikuwa yanasafirishwa nje ya nchi kutoka maeneo hayo kila siku, ambapo ilikuwa ni sawa na kuiba zaidi ya dola bilioni 2 kwa mwaka.

Nne: Vikwazo vya kiuchumi na 'Sheria ya Kaisari'

- Marekani haikutosheka na jinai hizo bali iliiwekea Syria vikwazo vikali vya kiuchumi na kupitisha "Sheria ya Kaisari" mwaka 2019. Vikwazo hivyo vilijumuisha kupiga marufuku miamala ya kifedha, kusimamisha mali na kutoa adhabu kwa mashirika yaliyokuwa yanashirikiana na serikali ya Syria. Matokeo ya vikwazo hivyo yalikuwa ni kuongezeka umaskini, uhaba wa dawa na chakula na mashinikizo makali kwa wananchi wa kawaida wa Syria hadi leo hii. Vikwazo hivyo vilisababisha ongezeko la asilimia 300 la bei ya dawa na chakula na kushuka kwa kasi thamani ya sarafu ya taifa ya Syria.

Kiujumla ni kwamba serikali ya wakati huo ya Syria iliishutumu Marekani mara kwa mara kwa kufanya uhalifu wa kivita na kukanyaga Hati ya Umoja wa Mataifa. Mashirika ya haki za binadamu kama vile Human Rights Watch na Amnesty International pia yalielezea wasiwasi mkubwa kuhusu jinai za Marekani nchini Syria. Hata hivyo, kutokana na ushawishi wa kisiasa wa Marekani, hakuna hatua za kisheria za kimataifa ambazo zimechukuliwa dhidi ya Washington hadi sasa.

Hitimisho: Urithi wa Umwagaji damu wa Uingiliaji wa Amerika

Uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Syria si tu haukuwasafisha magaidi wa Daesh (ISIS), lakini pia ulisababisha uharibifu mkubwa, kupotea roho za wanadamu, uporaji wa rasilimali na ukosefu wa utulivu wa kisiasa. Jinai hizo kwa kweli zimeingia kwenye kumbukumbu ya kihistoria ya wananchi wa Syria ambao wanasema kuwa huo ni uhalifu wa wazi dhidi ya binadamu, na madhara yake bado yanaonekana katika eneo hil hadi hivi sasa. Jinai hizo za Marekani hazikuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa tu, lakini pia hadi leo hii zinawatesa wananchi wa Syria hasa kimaisha, kiusalama na kiuchumi.