Araghchi: Trump amekiri kutenda jinai kwa kutishia kuwaua Wairani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema vitisho vipya vilivyotolewa na Rais Donald Trump vya kuwashambulia na kuwaua wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ni kukiri wazi wazi kwa kiongozi huyo wa Marekani juu ya kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Shirika la habari la Mehr limeripoti kuwa, Sayyid Abbas Araghchi ameeleza hayo katika barua aliyomtumia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa UN.
Ameeleza kuwa, vitisho hivyo ni ishara ya wazi na kukiri Trump kuwa serikali yake imefanya na inapanga kushadidisha jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu katika mashambulizi ya pamoja ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, yaliyoanza tangu Februari 28.
Araghchi amesema mashambulizi hayo ya kijinai ambayo yanalenga shule, hospitali, majengo ya makazi ya watu, viwanja vya michezo na miundomsingi mingine ya kiraia mpaka sasa yamepelekea kuuawa shahidi Wairani zaidi ya 1,300 wakiwemo watoto 160 wa Shule ya Msingi huko Minab.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha kuwa, hujuma za kinyama za Marekani na Israel mpaka sasa zimepelekea kuharibiwa maeneo 9,669 ya kiraia, yakiwemo majengo 7,943 ya makazi ya watu, vituo vya biashara 1,617, shule na vituo vya elimu zaidi ya 65, vituo 32 vya matibabu na dawa, na majengo 13 ya Shirika la Hilali Nyekundu la Iran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, jinai hizo, pamoja na vitisho vipya vilivyotolewa na Trump vya kuwashambulia na kuwaua wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ni kukiri wazi kiongozi huyo wa Marekani kwamba amefanya na ataendelea kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Amesema Iran itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kujilinda kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa, mpaka pale Baraza la Usalama la UN litakapotekeleza jukumu lake la kuidhaminia dunia amani na usalama.
Waziri Araghchi ameeleza bayana kuwa, Marekani inapasa kubebeshwa dhima na kuwajibishwa kulilipa fidia taifa la Iran kutokana na maafa na uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya kinyama yanayoendelea kufanya na Washington kwa ushirikiana na utawala haramu wa Israel.