Mufti Mkuu wa Russia ampongeza Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei
https://parstoday.ir/sw/news/world-i137288-mufti_mkuu_wa_russia_ampongeza_ayatullah_sayyid_mojtaba_khamenei
Mufti Mkuu wa Russia ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini ya Waislamu wa Shirikisho la Russia ametuma ujumbe akimpongeza Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kwa kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu.
(last modified 2026-03-11T08:38:30+00:00 )
Mar 11, 2026 08:38 UTC
  • Mufti Mkuu wa Russia ampongeza Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei

Mufti Mkuu wa Russia ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini ya Waislamu wa Shirikisho la Russia ametuma ujumbe akimpongeza Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kwa kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Sheikh Ravil Gaynutdin ameandika katika ujumbe huo kwamba: Kwa niaba ya Idara ya Masuala ya Kidini ya Waislamu wa Shirikisho la Russia, jamii ya Waislamu milioni 25 ya nchi hii, na mimi mwenyewe, ninakupongeza kwa kuchaguliwa katika nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na ninamuomba Mwenyezi Mungu akuwezeshe kubeba bendera ya Iran huru kwa heshima na ustahili na kuliongoza vyema taifa ndugu katika nchi hiyo.

Sehemu moja ya ujumbe huo inasema: Ninamuomba Mungu na ninatarajia kwamba utumishi wako mtukufu katika nafasi hii ya juu utaimarisha na kustawisha Iran, kuimarisha amani Mashariki ya Kati na kudumisha udugu miongoni mwa mataifa ya Kiislamu kote duniani.

Mufti Mkuu wa Russia ameendelea kusema: "Imekadiriwa wewe uchukue uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi kigumu na cha kihistoria. Ushike usukani wa nchi baada ya kuuawa shahidi baba yako mtukufu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye amepata daraja ya juu ya kuuawa shahidi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani huku akililinda taifa lake dhidi ya uvamizi wa kigeni... "

Ujumbe huo unaongeza: Daima ninaomba dua kwa ajili ya mustakabali mwema wa taifa la Iran na ninamuomba Mola wa walimwengu akupe nguvu na taufiki katika kuimarisha nguzo za dola, kutimiza wajibu mtakatifu wa kulinda ardhi yenu dhidi ya wavamizi, na kuimarisha umoja miongoni mwa raia wa Iran katika kukabiliana na adui, ili muwe imara katika mwanga wa wito wa Allah unaosema: “Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja wala msifarikiane” (Aal-Imran: 103).

Sheikh Gaynutdin amesema: "Natumai kwamba wakati wa uongozi wako, mchakato wa kukuza uhusiano kati ya Iran na Russia utaendelea kwa maslahi ya watu wa nchi hizo mbili."