Iran imeandaa maandamano makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137286-iran_imeandaa_maandamano_makubwa_ya_siku_ya_kimataifa_ya_quds
Maandamano makubwa ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds yanatarajiwa kufanyika katika miji na maeneo yote ya Iran Ijumaa hii.
(last modified 2026-03-11T06:10:04+00:00 )
Mar 11, 2026 06:10 UTC
  • Ramezan Sharif, mkuu wa Makao Makuu ya Siku ya Kimataifa ya Quds
    Ramezan Sharif, mkuu wa Makao Makuu ya Siku ya Kimataifa ya Quds

Maandamano makubwa ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds yanatarajiwa kufanyika katika miji na maeneo yote ya Iran Ijumaa hii.

Katika mji mkuu wa Iran, Tehran, wananchi watatembea hadi Chuo Kikuu cha Tehran, amesema Ramezan Sharif, mkuu wa Makao Makuu ya Siku ya Kimataifa ya Quds, katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Jumanne mjini Tehran.

Sharif amebaini kuwa zaidi ya wanahabari, wapiga picha na waandishi wa habari 6,000 wa ndani na nje ya nchi wataripoti maandamano hayo kote nchini.

Katika maelezo yake, Sharif amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo kinara na mbeba bendera wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Amefafanua kuwa wazo la kuanzisha Siku ya Kimataifa ya Quds limezuia kadhia ya Palestina na Al-Quds (Jerusalem) kusahaulika.

Akitaja siku hii kuwa ni siku ya umoja wa Waislamu, Sharif amesema imefichua sura halisi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na imetoa fursa ya kufufua mjadala kuhusu haki za Wapalestina pamoja na kuonesha ujasiri na uimara wao.

Akiashiria uvamizi wa pamoja wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, Sharif amesema huenda mojawapo ya malengo ya hujuma hiyo ni kugeuza uangalizi wa dunia kutoka kwa uhalifu unaofanywa na utawala wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Amesisitiza kwamba taifa la Iran litaibuka na ushindi kutoka katika vita hivi na litaushinda muungano wa Marekani na utawala wa Kizayuni.

Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa urithi ulioachwa na marehemu Imam Ruhollah Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye anaheshimiwa kama kiongozi wa kiroho na Waislamu duniani kote.

Mnamo mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoangusha utawala kiimla wa Shah aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani, Imam Khomeini alitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds.