Wananchi wa Uruguay waandamana wakitaka kukatwa uhusiano na Israel
Maelfu ya wananchi wa Uruguay waliingia mitaani na mabarabarani jana Ijumaa, kushiriki maandamano ya kuitaka serikali yao itambue mzozo wa kibinadamu unaoendelea Gaza kama mauaji ya halaiki, sanjari na kukata uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Israel.
Maandamano hayo ya nchi nzima, yaliyoandaliwa chini ya kaulimbiu "Imetosha kwa Mauaji ya Kimbari! Amani, Haki, na Uhuru," yalivutia maelfu katika maeneo yote 19 ya nchi, huku Montevideo ikitumika kama kitovu cha vuguvugu hilo.
Maandamano hayo yalichochewa zaidi na makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani kati ya Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas, ambayo pamoja na kutoa mwanga wa matumaini, yamekabiliwa na mashaka, huku wanaharakati wengi wakioyaona kuwa hayatoshi bila hatua madhubuti za kushughulikia masuala ya msingi.
Mjini Montevideo, waandamanaji walimiminika barabarani, wakipeperusha bendera za Palestina na kupiga nara kama vile "Ilikuwa hospitali, si kituo cha kijeshi!" na "Dola la Kizayuni, nyinyi ndio magaidi wa kweli!"
Zaidi ya Wayahudi 100 wa Uruguay walishiriki katika maandamano hayo, wakionyesha upinzani wao dhidi ya vitendo vya kinyama vya Israel huko Gaza. Mshiriki mmoja amesema, "Uzayuni ni itikadi ya ubaguzi wa rangi na sera yao kuu ni mauaji ya kimbari.
Agosti mwaka huu, serikali ya Uruguay iliamua kusitisha makubaliano ya ushirikiano yaliyotiwa saini mwezi Disemba mwaka jana 2024 kati ya Wakala wa Kitaifa wa Utafiti na Ubunifu wa Uruguay na chuo kikuu cha Israel huko Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu, sanjari na kufunga Ofisi yake ya Ubunifu mjini Jerusalem ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uruguay, Mario Lubetkin alitaja matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi na hatua za jeshi la Israel huko Gaza kuwa sababu za uamuzi huo. Kabla ya hapo, makundi mengi na mirengo ya kisiasa nchini humo yaliitaka serikali ya Rais wa Uruguay, Yamandu Orsi kuchukua msimamo mkali na madhubuti zaidi dhidi ya uvamizi wa Israel huko Gaza.