Je, Marekani ni nchi ya demokrasia au Jamhuri ya Mabilionea?
Ingawa karne moja iliyopita, ni asilimia 0.25 tu ya fedha za uchaguzi wa Marekani ndizo zilizotoka mifukoni mwa watu 100 matajiri zaidi wa nchi hiyo, lakini leo, dola moja kati ya kila dola 13 za chaguzi za serikali ya shirikisho hutoka moja kwa moja kwa mabilionea, jambo ambalo Washington Post imesema kuwa ni kuhodhiwa siasa za Marekani na mabilionea.
Marekani imeshuhudia mabadiliko makubwa ya muundo wa nguvu za kisiasa katika miaka ya hivi karibuni, mabadiliko ambayo matajiri wakubwa wamehodhi kila kitu na kuchukua nafasi za juu kabisa.
Gazeti la Washington Post limeiandikia makala maalumu maudhui hiyo chini ya kichwa cha maneno: "Jinsi Mabilionea Walivyoziteka Siasa za Marekani," na kutumia takwimu za kina kuonesha jinsi kundi la matajiri wachache lilivyohodhi kila kitu katika maamuzi na mustakbali wa makumi ya mamilioni ya raia wa Marekani. Maamuzi ya kijikundi hicho cha matajiri wachache ndicho hicho ambacho leo kinanadiwa kuwa ndiyo demokrasia yote duniani na dunia nzima wameanzisha vita, kuua watu kwa umati, kuharibu nchi za watu, kuzifukarisha na kufanya jinai nyingi za kivita kwa madai ya kusimamisha hiyo demokrasia ya kikundi hicho. Makala hiyo ya Washington Post imetegemea takwimu zilizofanyiwa uchunguzi wa kina ukijumuisha pia uchunguzi wa masuala ya kiuchumi na kutoa picha ya mfumo wa kisiasa wa Marekani ambao ushawishi wa kifedha umefunika si tu chaguzi muhimu sana bali umehodhi pia nguvu za utungaji sera na hata uteuzi wa mawaziri, viongozi na watumishi wa serikali.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, Wamarekani 100 matajiri zaidi walichangia asilimia 0.25 tu ya matumizi yote ya uchaguzi mkuu yaani uchaguzi wa shirikisho mwaka 2000. Lakini ilipofika mwaka jana 2024, takwimu hiyo ilikuwa imeongezeka mno na kufikia hadi asilimia 7.5 yaani kikundi hicho cha matajiri wa Marekani kilitumia zaidi ya dola bilioni 1.1 kudhibiti uchaguzi na kuamua nani awe rais na nani ashike nafasi zipi muhimu za uongozi.
Michango ya wastani ya kila mwaka ya kundi hilo la matajiri wachache wa Marekani kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 ilikuwa takriban dola milioni 21, lakini katika muongo mmoja uliopita, yaani kuanzia mwaka 2010 na kuendelea, fedha hizo zimeimeongezeka kwa kasi na kufikia kiwango cha juu kabisa mwaka jana, 2024. Ongezeko hilo la ajabu linaonesha jinsi vyama vya siasa vya Marekani vilivyo tegemezi kwa mabilionea wa nchi hiyo na jinsi mabilionea hao wachache wanavyohodhi masuala ya siasa, uongozi na maamuzi yote ya serikali za Marekani. Kwa kweli, Wamarekani 100 matajiri zaidi wana ushawishi mkubwa kwenye chaguzi za Marekani. Ushawishi huo si wa kifedha tu, bali pia ni wa kiitikadi na kimuundo. Mwaka 2024, zaidi ya asilimia 80 ya michango ya matajiri zaidi 100 wa Marekani ilikwenda kwa chama cha Republican cha Donald Trump na kuviinua na kuvifaidisha vigenge vyake vyenye siasa kali za kihafidhina. Michango hiyo ndiyo iliyomuangusha Biden na kumrejesha madarakani Trump. Mabadiliko makubwa yalianza kuonekana zaidi mwaka 2020 wakati mabilionea wa sekta za teknolojia na fedha walipoamua kumuunga mkono Trump na chama chake na kukipiga na chini chama cha Democratic. Elon Musk, mtu tajiri zaidi duniani, alitoa dola milioni 294 kumsaidia Trump na Warepublican katika uchaguzi wa rais pekee, na katika mkabala wake akapewa kifurushi chake cha mshahara wa dola trilioni 1 na Tesla.
Takwimu zinaonesha kuwa ushawishi huo wa mabilionea wachache huko Marekani umejikita zaidi katika muundo mkuu wa utawala nchini humo. Tangu mwaka 2010, maamuzi ya mahakama kama vile Citizens United dhidi ya Tume ya Uchaguzi ya Shirikisho yameruhusu vyama vya wafanyakazi na makampuni kutumia pesa bila ya mipaka. Matokeo yake ni kwamba kwa uchache mabilionea 44 au wenzi wao wamepata fursa za kugombea nafasi za majimbo au za serikali ya shirikisho tangu mwaka 2015 huko Marekani.
Baraza la mawaziri la Trump pia ndilo baraza la mawaziri lenye matajiri wengi zaidi katika historia yote ya Marekani. Lina watu wenye utajiri wa dola trilioni 7.5, na linajumuisha mabilionea kadhaa. Kihistoria, jambo hilo linakumbushia Enzi za Gilded, wakati utajiri ulipokuwa umelimbikizwa wote mikononi mwa watu wachache tu.
Leo, mabilionea 902 wa Marekani wanamiliki mali zaidi ya dola trilioni 6.7, yaani mara mbili ya mfumuko wa bei wa muongo mmoja uliopita. Hayo yote ni matokeo ya mapinduzi ya kiteknolojia. Trump aliahidi mwaka 2016 kuwa angeliwakandamiza wasomi, lakini katika muhula wake wa pili madarakani, mabilionea wamepata ushawishi wa wazi katika Ikulu ya White House.
Matokeo yake ni kuanguka imani ya umma kuhusu uadilifu, utendaji na haki ndani ya taasisi za Marekani. Uchunguzi wa maoni wa Washington Post wa mwaka 2024 uligundua kuwa Wamarekani wengi wanaamini kwamba matumizi ya mabilioni ya dola kwenye chaguzi za Marekani ni kitu kibaya sana huku asilimia 12 tu wakiamini kwamba ni kitu kizuri. Hali hiyo imeisukuma demokrasia ya Marekani kwenye shimo la udhibiti wa watu wachache. Mabilioni hayo ya fedha yanayomwagwa kwenye siasa za Marekani si tu huzifanya chaguzi za nchi hiyo kuwa na gharama kubwa mno, lakini pia huishia kwenye kuundwa sera zinazowapendelea wachache na kuwakandamiza makumi ya mamilioni ya wengine. Wakati wa kampeni za uchaguzi, Trump alikusanya pesa mara 15 zaidi kutoka kwa matajiri mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka 2016 na Kamala Harris wa chama cha Democratic alikusanya mara tatu zaidi kuliko alivyokusanya Hillary Clinton mwaka 2016. Kama hali hiyo haitodhibitiwa, basi hakuna kitakachozuia kutokea mageuzi ya kimsingi ambayo yatazidi kuibadilisha Marekani kuwa "jamhuri ya mabilionea," na si nchi ya kidemokrasia inayopaswa kuwa ya kuwahudumia watu bila ya ubaguzi wala unyonyaji wowote.