Yemen: Tunasimama na Lebanon na wapiganaji wa muqawama nchini humo
Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya Ansarullah ya Yemen imesisitiza uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Lebanon dhidi ya uvamizi na uchokozi wa mara kwa mara wa utawala ghasibu wa Kizayuni.
Katika taarifa yake kwa mnasaba wa kuzikwa shahidi Haitham Tabatabai, mmoja wa makamanda mashuhuri wa Hizbullah aliyeuawa kigaidi hivi karibuni na utawala wa Kizayuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ansarullah ya Yemen imesisitiza kuwa, kamanda huyo alikuwa na nafasi muhimu katika kulinda usalama na umoja wa ardhi ya Lebanon na kuunga mkono mhimili wa mapambano ya ukombozi wa ardhi za Kiislamu. Imeelezwa katika taarifa hiyo kwamba siasa za ugaidi na jinai za utawala wa Kizayuni zinaonyesha utawala huo kushindwa na kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na mahasimu wake katika medani za vita. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Yemen imesikitishwa na njama pamoja na ushirikiano wa baadhi ya tawala za Kiarabu na Kiislamu na utawala wa Tel Aviv na vile vile kimya cha kimataifa kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Lebanon na Palestina.
Kinyume na nchi nyingine za Kiarabu, na licha ya uwezo wake mdogo wa kifedha, Yemen imekuwa katika mstari wa mbele katika kutetea na kuwaunga mkono wananchi madhlumu wa Ukanda wa Gaza na vilevile Lebanon.