OXFAM: Nusu ya raia Sudan Kusini wanakabiliwa na njaa kali
-
Njaa kali yaiathiri Sudan Kusini
Shirika la OXFAM limetangaza kuwa, takriban watu milioni sita wanakabiliwa na baa la njaa kali Sudan Kusini, idadi ambayo ni sawa na nusu ya raia wote nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika hilo, watu wa Sudan Kusini wanakabiliwa pia na huduma duni ya maji safi. Imeelezwa kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kali inatarajiwa kupanda hadi kufikia milioni 7.5 ifikapo mwezi Aprili mwakani.
Oxfam imesema hadi sasa ni asilimia 40 pekee ya dola bilioni 1.6 za mpango wa msaada kwa taifa hilo changa zaidi barani Afrika ndiyo ambayo imeshatolewa. Upungufu huo unatokana na mataifa ya Magharibi kupunguza bajeti zao za misaada.
Sudan Kusini ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi cha miaka mitano hali iliyosababisha zaidi ya raia milioni 2 kuyahama makazi yao. Nchi hiyo licha ya hali ngumu inawahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka taifa jirani la Sudan lialokabiliwa na vita.
Septemba mwaka huu upinzani nchini Sudan Kusini ulitoa wito wa "mabadiliko ya utawala" dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir baada ya miezi kadhaa ya kuvunjika kwa makubaliano ya kugawana madaraka mwaka 2018 na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar.
Mivutano na hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kati ya pande mbili za Rais Salva Kiir na Machar na ikashtadi mnamo mwezi Februari mwaka huu wakati kundi liitwalo Jeshi Jeupe ambalo ni tiifu kwa Machar, lilipovamia kambi ya jeshi jimboni la Upper Nile na kushambulia pia helikopta ya Umoja wa Mataifa.