Wakimbizi 115 wa Burundi warudishwa nyumbani kutokea Rwanda
Wakimbizi 115 wa Burundi, ambao wengi wao walikuwa wamekimbilia Rwanda mwaka huu wa 2015 kutokana na machafuko ya kisiasa nchini mwao, wamerudishwa kwa hiari nchini Burundi. Hayo ni kwa mujibu wa Wizara ya Usimamiaji wa Masuala ya Dharura ya Rwanda.
Kundi hilo limejumuisha watu 107 kutoka Kambi ya Wakimbizi ya Mahama katika Wilaya ya Kirehe mashariki mwa Rwanda, na wengine wanane ni kutoka Kigali, mji mkuu wa Rwanda.
Gonzague Karagire, meneja wa ratiba ya wakimbizi katika wizara hiyo ya Rwanda amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, wakimbiizi hao wamekabidhiwa kwa mamlaka za Burundi katika mpaka wa Rwanda na Burundi huko Nemba.
Karagire amewaambia waandishi wa habari kwamba kurejea wakimbizi hao ni kwa hiari, na wakati wowote watakapoamuakurudi nchini kwao basi jukumu la serikali ya Rwanda litakuwa ni kuwezesha kurudi salama nyumbani kwao.
Wizara hiyo pia imesema: "Kwa sasa Rwanda ina wakimbizi 52,862 wa Burundi, wakiwemo 42,421 katika kambi ya Mahama na wengine katika maeneo ya mijini."
Mwezi Januari mwaka huu 2025, Burundi ilikata uhusiano na kufunga mpaka wake na Rwanda baada ya kuishutumu Kigali kuwa inawapa hifadhi waasi wa RED-Tabara. Rwanda ilikanusha madai hayo.
Wakimbizi wa Burundi wanarejea kwa hiari nchini kwao kutokea Rwanda katika hali ambayo nchi hiyo ya Burundi yenyewe ni kimbilio la makumi ya maelfu ya wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Congo.
Taarifa zilizotolewa mwezi Machi mwaka huu zilisema kuwa, zaidi ya watu 60,000 walivuka mpaka na kuingia Burundi katika muda wa wiki mbili tu, wakikimbia ghasia na machafuko makubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).