Waangalizi wa uchaguzi walaani mapinduzi ya kijeshi Guinea-Bissau
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133664-waangalizi_wa_uchaguzi_walaani_mapinduzi_ya_kijeshi_guinea_bissau
Viongozi wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) pamoja na Jukwaa la Wazee wa Afrika Magharibi (WAEF) wameeleza “wasiwasi mkubwa” kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Guinea-Bissau baada ya uchaguzi wa urais.
(last modified 2025-11-27T16:50:50+00:00 )
Nov 27, 2025 12:23 UTC
  • Waangalizi wa uchaguzi  walaani mapinduzi ya kijeshi Guinea-Bissau

Viongozi wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) pamoja na Jukwaa la Wazee wa Afrika Magharibi (WAEF) wameeleza “wasiwasi mkubwa” kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Guinea-Bissau baada ya uchaguzi wa urais.

Jeshi lilimng’oa madarakani Rais Umaro Sissoco Embaló siku ya Jumatano, wakati taifa hilo likisubiri matokeo ya kura za uchaguzi wa urais na bunge uliofanyika Jumapili.

Katika taarifa ya pamoja, ujumbe wa waangalizi ulisema: “Ni jambo la kusikitisha kwamba tangazo hili limetolewa muda mfupi baada ya kukutana na wagombea wakuu wawili wa urais, ambao walituhakikishia utayari wao kukubali matakwa ya wananchi.”

Kundi la maafisa wa kijeshi waliotambulisha kama “Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Urejeshaji wa Usalama wa Taifa na Utulivu wa Umma” lilitangaza kupitia televisheni ya taifa kwamba limechukua mamlaka yote ya dola.

Jeshi lilisitisha shughuli zote za vyombo vya habari, likasimamisha mchakato wa uchaguzi, kufunga mipaka na kutangaza kafyu ya saa tisa kuanzia saa tatu usiku kwa saa za eneo.

Viongozi wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi waliitaka AU na ECOWAS kuchukua hatua za haraka kurejesha utaratibu wa kikatiba. Pia walieleza wasiwasi kuhusu kukamatwa kwa maafisa waliokuwa wakisimamia mchakato wa uchaguzi.

Awali, waangalizi hao wa uchaguzi walikuwa wamewapongeza wananchi wa Guinea-Bissau kwa mshikamano wao na kusema upigaji kura ulifanyika kwa utulivu na kwa amani.

Mapinduzi hayo ya kijeshi yametokea wakati mgombea huru Fernando Dias na ile ya Rais Embaló wote walidai ushindi Jumatatu, huku taifa likisubiri matokeo rasmi.

Jumla ya wagombea 12 walikuwa wakishindania urais, na tume ya uchaguzi ilikuwa imetarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho kufikia Alhamisi.