Iran yawaonya mahasimu kuhusu mbinu za mabavu na mashinikizo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133662-iran_yawaonya_mahasimu_kuhusu_mbinu_za_mabavu_na_mashinikizo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ametoa onyo kali kwa mahasimu wa Jamhuri ya Kiislamu akiwataka waache mwenendo wa mabavu na mashinikizo ya kupita kiasi dhidi ya taifa hili.
(last modified 2025-11-27T16:52:12+00:00 )
Nov 27, 2025 12:22 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi (kulia), na  mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot
    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi (kulia), na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ametoa onyo kali kwa mahasimu wa Jamhuri ya Kiislamu akiwataka waache mwenendo wa mabavu na mashinikizo ya kupita kiasi dhidi ya taifa hili.

Aragchi ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, siku ya Jumatano mjini Paris, ambako alisafiri kwa mwaliko wa afisa huyo wa Kifaransa.

Araghchi amewataka wahusika wa uhasama huo kuachana na “mbinu za mabavu na za kupita kiasi” huku akiwataka wabebe dhima ya matendo yao.

Kama mifano ya wazi ya mwenendo huo, alitaja kujiondoa kwa Marekani mnamo mwaka 2018 kutoka makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, (JCPOA), yaliyosainiwa kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani. Pia ameashiria vita visivyo halali na vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, ikiwemo mashambulizi ya Juni dhidi ya vituo vya nyuklia.

Amesema tawala za Marekani na Israel zimekiuka sheria za kimsingi za kimataifa kwa uchokozi wao dhidi ya Iran.

Araghchi amesisitiza haki ya kisheria ya Iran kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na akasisitiza dhamira njema na umakini wa Jamhuri ya Kiislamu kushiriki mazungumzo ya busara na yenye mantiki ili kubaini uhakika kuhusu malengo ya amani ya mpango wake wa nyuklia.

Hata hivyo, ameonya kuwa Iran haitavumilia uvunjaji wa mamlaka yake ya kujitawala au mashambulizi dhidi ya vituo vyake vya nyuklia ambavyo vina kinga ya sheria za kimataifa.

Waziri huyo pia ameikosoa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwa hatua zao dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

Alikuwa akiashiria juhudi za mataifa hayo matatu kujaribu kufufua vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran na kushinikiza mara kadhaa Bodi hiyo kutoa maazimio ya kupinga Iran, licha ya wao wenyewe kukiuka makubaliano yao ya nyuklia na kiuchumi kuhusu Jamhuri ya Kiislamu.

Araghchi amazitaja nchi hizo tatu kuwa chanzo cha kuongezeka mvutano na akaitaka IAEA kuchukua msimamo huru unaozingatia sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), unaotambua haki ya mataifa kuendeleza nishati ya nyuklia kwa amani.

Aidha, Araghchi amelaani uhalifu na vitendo vya uvamizi vinavyoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina, Walebanoni na watu wengine wa eneo hilo.

Amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kulinda utawala wa sheria, kutetea haki za Wapalestina na kuhakikisha heshima ya mamlaka na mipaka ya kila taifa.