Rais wa Nigeria atangaza hali ya hatari kufuatia wimbi la utekaji nyara
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133666-rais_wa_nigeria_atangaza_hali_ya_hatari_kufuatia_wimbi_la_utekaji_nyara
Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ametangaza hali ya hatari ya kiusalama nchini humo baada ya mauaji na utekaji nyara kuongezeka kwa kasi.
(last modified 2025-11-27T12:25:24+00:00 )
Nov 27, 2025 12:25 UTC
  • Rais wa Nigeria, Bola Tinubu
    Rais wa Nigeria, Bola Tinubu

Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ametangaza hali ya hatari ya kiusalama nchini humo baada ya mauaji na utekaji nyara kuongezeka kwa kasi.

Katika taarifa iliyotolewa Ikulu na kusambazwa kupitia mtandao wa X siku ya Jumatano, Rais huyo wa Nigeria ameliagiza Jeshi la Polisi kuongeza askari wapya 20,000 ili kukabiliana na hali inayozorota ya usalama, na kufanya idadi ya askari wapya watakaoajiriwa kufikia 50,000. Jumapili iliyopita tayari alikuwa ametoa maelekezo ya kuajiri askari polisi 30,000.

Rais Tinubu amesema: Ingawa nilishapitisha mpango wa kuboresha vituo vya mafunzo ya polisi kote nchini, kwa tangazo hili polisi wanaruhusiwa kutumia kambi za Huduma ya Vijana kwa Taifa kama vituo vya mafunzo.”

Aidha, askari waliokuwa wakihudumu kama walinzi wa watu mashuhuri (VIP) wataondolewa na kupatiwa mafunzo ya haraka ili waweze kutumwa katika maeneo yenye changamoto za kiusalama.

Rais Tinubu pia ameagiza Idara ya Usalama wa Taifa (DSS) kupeleka walinzi wa misitu waliopatiwa mafunzo maalum ili kuwakamata na kuwatimua magaidi wanaojificha katika mapori.

Akihutubia taifa, Rais Tinubu amesema: “Wenzangu Wanaigeria, hii ni hali ya hatari ya kitaifa. Tunajibu kwa kuongeza askari , hususan katika maeneo yenye changamoto za kiusalama. Nyakati hizi zinahitaji mshikamano wa kila mmoja wetu. Tushirikiane kulinda taifa letu.”  

Rais Tinubu amelitaka Bunge la Taifa kuangalia upya sheria ili kuruhusu majimbo kuanzisha polisi wa majimbo pale inapohitajika. Vilevile, amewahimiza viongozi wa mitaa na taasisi za kidini kuimarisha hatua za usalama.

Pia amewataka wananchi wasikate tamaa wala kuogopa, akisisitiza kuwa serikali imejizatiti kulinda raia, kudumisha mshikamano wa kitaifa na kusaidia vikosi vya usalama kurejesha amani.

Rais Tinubu ametoa wito kwa wananchi waripoti harakati zozote zenye kutiliwa shaka huku akiwataka washirikiano na vyombo vya usalama na kuongeza kuwa:  "Hivi ni vita vyetu sote, na kwa mshikamano tutashinda.”

Wiki iliyopita zaidi ya wanafunzi 300 walitekwa kutoka shule ya Kikatoliki katika jimbo la Niger, kaskazini ya kati mwa nchi hiyo.

Mapema mwezi huu, Rais wa Marekani Donald Trump alitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Nigeria kwa madai ya mauaji ya Wakristo. Serikali ya Nigeria imepinga madai hayo, ikiyataja kuwa ni taswira potofu ya hali halisi. Serikali ya Nigeria inasema raia wote wa nchi hiyo, wawe Wakristo au Waislamu ni waathirika wa mashambulizi ya magaidi na watekaji nyara.