Muqawama: Hatutaruhusu Palestina iwe ngome ya mamluki wa Kizayuni
Makundi ya Muqawama ya Palestina yamepongeza operesheni ya kuzisafisha taasisi za usalama katika Ukanda wa Ghaza, na kutangaza kuwa Palestina kamwe haitakuwa kimbilio na ngome ya mamluki wa adui Mzayuni.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Shihab, makundi ya Muqawama ya Palestina yamesema katika taarifa kuwa: "Tunapongeza operesheni za kiusalama za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wakala wa Usalama wa Taifa katika Ukanda wa Ghaza kwa ajili ya kutekeleza mashitaka ya wavunja sheria, mamluki, majambazi na wale wanaoshirikiana na adui Mzayuni."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Tunasisitiza kuwa operesheni za usalama za Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa zinaungwa mkono na makundi yote ya Palestina, na operesheni hii yenye lengo la kurejesha usalama na uthabiti na kusambaratisha magenge ya mamluki, wahalifu na wafuasi wa adui Mzayuni, inaungwa mkono na taasisi za usalama za Muqawama."
Makundi ya Muqawama wa Palestina yameongeza kusema: "Tunawaomba raia wote kushirikiana na vyombo vya usalama na Wizara ya Mambo ya Ndani na kutoa taarifa kuhusiana na watu wanaosakwa na wafuasi wao. Tunasisitiza kuwa, kuwaficha watoro na wahalifu ni uhalifu wenyewe."
Taarifa hiyo imebainisha kuwa: "Ujumbe wetu kwa magenge yote ya wahalifu wanaoshajiishwa na ufadhiliwa na utawala wa Kizayuni na idara zake za kijasusi ni kwamba, (Palestina) si mahali pa mamluki, makatili, majambazi na yeyote atakayethibitika kuhusika na jinai hizo ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya mapinduzi ya Palestina, na hakuna atakayesalimika."
Jabaliya, mji ulioko kaskazini mwa Ghaza, limekuwa eneo la mapigano makali kati ya wapiganaji wa Muqawama na magenge ya mamluki wanaoshirikiana na vikosi vamizi vya Israel tangu Jumanne asubuhi.