Burkina Faso, Mali na Niger zatangaza kujiondoa ICC
Mataifa ya Afrika Magharibi ya Burkina Faso, Mali na Niger yametangaza kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kusema mahakama hiyo ni chombo cha ubeberu cha "Ukoloni Mamboleo".
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi tatu za Burkina Faso, Mali na Niger imeeleza kuwa Mahakama ya ICC yenye makao yake makuu mjini Hague Uholanzi ni chombo la ukandamizaji cha Ukoloni Mamboleo kinachodhibitiwa na mabeberu wa dunia.
Viongozi wa nchi hizo tatu za magharibi mwa Afrika wamesema kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imethibitisha yenyewe kuwa haina uwezo wa kushughulikia, kuchunguza na kutoa hukumu kwa jinai zilizothibitishwa, jinai dhidi ya binadamu, jinai za mauaji ya kimbari na jinai za ukandamizaji.
Burkina Faso, Mali na Niger pia zimeeleza kuwa zinataka kuasisi mfumo wa asili kwa ajili ya kuimarisha amani na uadilifu.
Inafaa kuashiria hapa kuwa nchi za Magharibi mwa Afrika zimeathiriwa na hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani unaosababishwa na makundi ya kigaidi yenye mfungamano na al Qaida na Daesh (ISIS).
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilianzishwa mwaka 2002 lengo likiwa ni kuchunguza na kuwafungulia mashtaka wahalifu wa kivita.