Chanjo erevu iliyotengenezzwa Iran kutibu Saratani ya Mapafu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i131168-chanjo_erevu_iliyotengenezzwa_iran_kutibu_saratani_ya_mapafu
Mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran ametangaza chanjo yenye akili mnemba (AI) kwa ajili ya kutibu saratani ya mapafu.
(last modified 2025-09-24T02:15:06+00:00 )
Sep 24, 2025 02:15 UTC
  • Chanjo erevu iliyotengenezzwa Iran kutibu Saratani ya Mapafu

Mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran ametangaza chanjo yenye akili mnemba (AI) kwa ajili ya kutibu saratani ya mapafu.

Saratani ya mapafu ni miongoni mwa aina hatari zaidi za saratani duniani, na juhudi za kisayansi za kutafuta mbinu mpya na madhubuti za matibabu zinaendelea kwa kasi. Katika muktadha huu, Daktari Mohammad Hossein Yazdi, Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Bioteknolojia katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran na Mhadhiri Mwandamizi katika Kitivo cha Famasia cha Iran, amepiga hatua kubwa katika kutegeneza chanjo za kisasa dhidi ya saratani.

Dkt. Yazdi alieleza kuwa chanjo hiyo ya kiubunifu imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya mRNA pamoja na algorithimu za utabiri zinazotegemea akili mnemba. Mbinu hii huwezesha chanjo kubuniwa kwa usahihi mkubwa kulingana na vinasaba vya uvimbe wa kila mgonjwa.

Akaongeza kuwa njia hii ya kiteknolojia inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa utafiti na maendeleo, na kufungua milango mipya ya tiba na kinga dhidi ya saratani ya mapafu.

Kwa mtazamo wa Dkt. Yazdi, mojawapo ya sifa kuu za chanjo hii ni uwezo wake wa kutabiri kwa usahihi. Tofauti na chanjo za jadi zinazohitaji majaribio ya muda mrefu, chanjo hii mahiri hutumia data za vinasaba vya uvimbe wa wagonjwa pamoja na algorithimu za hali ya juu za akili mnemba ili kubaini wanaohitaji chanjo kabla ya kuanza majaribio ya kitabibu. Njia hii huweza kuharakisha mchakato wa maendeleo ya chanjo kwa takriban asilimia 90, na kupunguza muda wa kubuni na kuandaa chanjo hiyo hadi wiki mbili au tatu tu.

Dkt. Yazdi alisisitiza kuwa ubinafsishaji wa chanjo si tu kwamba unatoa fursa ya matibabu kwa wagonjwa wa saratani, bali pia unaweza kuwa kinga kwa wale walio katika hatari. Sifa hii huibadilisha chanjo kutoka kuwa bidhaa ya kawaida hadi kuwa chombo cha kisasa katika tiba sahihi, na kutoa matumaini ya mageuzi makubwa katika matibabu ya saratani ya mapafu.