Tshisekedi: DRC haitapiga mnada rasilimali zake kwa Marekani
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Félix Tshisekedi, ametangaza kuwa licha ya msaada wa Marekani katika upatanisho wa migogoro, nchi yake haitauza kwa bei rahisi au kupiga mnada rasilimali zake kwa taifa hilo la Magharibi.
Serikali ya Rais Donald Trump imedai kuwa eti na hamu ya kumaliza mapigano ya umwagaji damu mashariki mwa DRC. Aidha Trump ametangaza kuwa atawekeza mabilioni ya dola katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DRC, huku tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa makubaliano hayo ikipangwa mwezi huu.
Rais Tshisekedi ameshiria mwelekeo huo wa Marekani na kusema: serikali yaek itashirikiana katika kuendeleza sekta ya madini na kujenga miundombinu.
Aidha, alibainisha kuwa DRC tayari imesaini ushirikiano wa kimkakati na China, na kwa sasa inaendelea na mazungumzo ya kufikia makubaliano kama hayo na Marekani.
Hata hivyo, Tshisekedi amesisitiza kuwa makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani kati ya Rwanda na DRC, yaliyotiwa saini tarehe 27 Juni, hayajafaulu kupunguza mapigano mashariki mwa Kongo.
Nchi ya Kongo hususan mashariki mwa nchi hiyo, imejaa madini na utajiri mkubwa wa kimaumbile ambao unakodolewa macho na nchi mbalimbali kwa miongo kadhaa, na suala hilo linahesabiwa kuwa moja ya sababu za vita vya sasa mashariki mwa nchi hiyo.
Weledi wa mambo wanasema Trump, ambaye ana historia ndefu katika nyanja za shughuli za kiuchumi na kibiashara, anataka kunyonya migodi yenye thamani kubwa duniani kote katika utawala wake kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi ya Marekani au makampuni ya nchi hiyo. Katika mkondo huo, anatumia masuala ya kulinda usalama kwa ajili ya kudhibiti sehemu kubwa ya masoko ya kimataifa yajayo kwa kupata umiliki au hisa kubwa ya migodi ya madini hasa madini adimu, ili kuimarisha nafasi ya Marekani duniani.