Sababu za kuongezeka maradufu mauzo ya Iran barani Afrika
Mauzo ya Iran barani Afrika yameongezeka maradufu.
Mnamo Septemba 15, Mohammad Reza Safari, mkuu wa Ofisi ya Afrika ya Shirika la Maendeleo ya Biashara la Iran alitangaza kuwa katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu wa Kiirani, mauzo ya nje ya Iran katika bara la Afrika yameongezeka mara mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, na wakati huo huo kupungua kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Aliongeza kuwa kutokana na uwezo wa mikoa ya Iran, wazalishaji katika maeneo hayo wamehimizwa kunufaika na fursa za uzalishaji wa pamoja katika nchi za Kiafrika na hivyo kuidhaminia nchi fedha za kigeni.
Huku akifafanua kuwa Afrika inahitajia mitambo, mashine na viwanda katika nyanja za kilimo, Safari ameongeza kuwa makampuni ya Iran yana uwezo unaohitajika kwa ajili ya kushirikiana na wakulima na wahusika wengine katika uwanja huo na kwamba kwa sababu hiyo, Kitengo cha Afrika kinaunga mkono miradi ya pamoja ya uzalishaji barani Afrika na kimebuni nyenzo zinazohitajika kwa ajili ya kutoa suhula kwa makampuni ya Iran.
Masoud Barhaman, Mkuu wa Jumuiya ya Biashara ya Pamoja ya Iran na Afrika Mashariki pia alisisitiza tarehe 6 Septemba kwamba takwimu rasmi zinaonyesha ongezeko kubwa la mara 2.2 katika kipindi cha miezi 4 ya mwanzo wa mwaka wa Kiirani na kusema: 'Idadi ya vituo pia imeongezeka kutoka nchi 29 hadi 34. Kwa mujibu wa data rasmi za hivi karibuni zilizotangazwa na Idara ya Forodha, katika miezi 3 ya kwanza ya mwaka wa Kiirani, mauzo ya nje ya Iran kwenda Afrika yalikuwa ya karibu dola milioni 260, kiwango ambacho kimekuwa kwa asiimia 85 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Barhaman aliendelea kusema: 'Kwa hiyo, kwa mujibu wa mwenendo wa miezi 4 ya kwanza ya mwaka huu, tunaweza kusema kwamba katika miezi 5 ya kwanza ya mwaka, biashara ya Iran na Afrika imeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita, ingawa idadi kamili ya miezi 5 bado haijachapishwa. Amesisitiza kuwa, iwapo hakutakuwa na matukio yasiyotabirika, inatazamiwa kuwa mwenendo wa mabadilishano ya biashara ya Iran na Afrika utaendelea kuongezeka katika nusu ya pili ya mwaka, ingawa si kwa kasi ya miezi 4 ya mwanzo, bali katika ukuaji thabiti zaidi na unaoshuka na kupanda.

Kwa mujibu wa wataalamu, mambo muhimu ambayo yamepelekea kuongezeka biashara kati ya Iran na Afrika ni pamoja na uzingatiaji zaidi wa Shirika la Maendeleo ya Biashara kwa bara la Afrika na kuandaliwa ramani ya njia kwa kushauriana na sekta binafsi, kuboreka kwa huduma za forodha, kuingia huduma za uhandisi wa kiufundi katika soko hili na kutiwa saini mikataba muhimu, maelewano kati ya makundi yanayojishughulisha barani Afrika na uwepo hai wa vyumba vya pamoja vya biashara kati ya Iran na Afrika.
Wakati huo huo, sababu za kuongezeka mauzo ya Iran barani Afrika zinaweza kuorodheshwa kama ifuatavyo:
1. Diplomasia hai ya Iran barani Afrika
Kufanyika mikutano ya kilele ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Afrika na utekelezaji wa mapendekezo yanayopitishwa na Kitengo cha Afrika umekuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara wa pande mbili. Hatua hizi zimeongeza kuaminiana na kuwezesha michakato ya biashara kati ya pande hizi.
2. Bidhaa tofauti zinazouzwa nje ya nchi
Mauzo ya Iran barani Afrika yanajumuisha bidhaa zenye thamani ya juu kama vile bidhaa za petrokemikali, saruji, bidhaa za reli, dawa, vifaa vya matibabu, vifaa vya ujenzi, vya nyumbani na chakula. Utofauti huu wa bidhaa umezivutia nchi nyingi katika bara la Afrika.
3. Matumizi na mabadilishano ya fedha za ndani
Ili kupunguza utegemezi wa mifumo ya fedha ya kimataifa na kukabiliana na vikwazo vya sarafu, Iran inatumia njia ya sarafu za ndani katika kubadilishana biashara na nchi za Afrika. Mbinu hii imerahisisha miamala na kupunguza gharama za kifedha.
4. Kuboresha miundombinu ya uchukuzi
Ustawishaji na uboreshaji wa njia za usafiri wa baharini hususan kupitia bandari za Iran hadi nchi za Afrika Mashariki na Magharibi kumepunguza sana gharama za uchukuzi na kurahisisha ufikishaji wa bidhaa katika masoko ya Afrika.
5. Mahitaji makubwa ya Afrika kwa bidhaa za msingi
Migogoro ya kimataifa ya chakula na nishati imeongeza mahitaji ya Afrika kwa bidhaa za kimsingi kama vile mbolea, saruji, chakula na dawa. Kwa kudhamini mahitaji haya, Iran imeweza kuimarisha nafasi yake katika masoko ya Afrika.
Kwa kumalizia, tunaweza kusema kuwa, ukuaji wa mauzo ya Iran barani Afrika ni matokeo ya mchanganyiko wa diplomasia amilifu, uanuwai wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi, matumizi ya mbinu za kisasa za kifedha, uboreshaji wa miundombinu ya uchukuzi na kudhaminiwa mahitaji ya kimsingi ya soko la Afrika. Kwa kuendelezwa mchakato huu na kuondolewa vizingiti vilivyopo, tunaweza kutarajia kuwa uhusiano wa kibiashara wa Iran na bara la Afrika utaimarika na kupanuka zaidi katika siku za usoni.