Mabadiliko ya tabianchi; vimbunga vya vumbi vimeathiri watu milioni 330 duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128242-mabadiliko_ya_tabianchi_vimbunga_vya_vumbi_vimeathiri_watu_milioni_330_duniani
Ripoti mpya ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) imebainisha kuwa, dhoruba za mchanga na vumbi zinaongoza kwa "vifo vya mapema" kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ambapo zaidi ya watu milioni 330 katika nchi 150 wameathirika.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Jul 12, 2025 14:09 UTC
  • Mabadiliko ya tabianchi; vimbunga vya vumbi vimeathiri watu milioni 330 duniani

Ripoti mpya ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) imebainisha kuwa, dhoruba za mchanga na vumbi zinaongoza kwa "vifo vya mapema" kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ambapo zaidi ya watu milioni 330 katika nchi 150 wameathirika.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) leo Jumamosi limeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dhoruba za Mchanga na Vumbi, na kuainisha mwaka 2025 - 2034 kuwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Dhoruba za Mchanga na Vumbi.

Dhoruba "zimegeuka na kuwa moja ya changamoto za ulimwengu ambazo hazizingatiwi lakini kubwa za enzi zetu", amesema Rais wa baraza hilo, Philemon Yang.

"Vimbunga hivyo vinatokana na mabadiliko ya hali ya hewa, uharibifu wa ardhi na mazoea yasiyo endelevu." Katibu Mkuu wa WMO, Celeste Saulo, alisema Alkhamisi kwamba, dhoruba za mchanga na vumbi hazimaanishi tu "madirisha machafu na anga yenye giza.

Ameongeza kuwa zinadhuru afya na ubora wa maisha ya mamilioni ya watu na kugharimu mamilioni ya dola kupitia usumbufu wa usafiri wa anga na ardhi, na kwenye kilimo na uzalishaji wa nishati ya jua.

Chembechembe za hewa kutoka kwa dhoruba hizi huchangia vifo vya mapema vipatavyo milioni 7 kila mwaka, amesema Yang, akiongeza kuwa husababisha magonjwa ya kupumua na ya moyo na mishipa, na kupunguza mavuno ya mazao kwa hadi 25%, na kusababisha njaa na watu kuhama.

"Takriban tani bilioni 2 za vumbi huzalishwa kila mwaka, sawa na mapiramidi 300 za Giza" nchini Misri, Laura Paterson, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa wa WMO, aliuiambia mkutano wa UNGA.

Zaidi ya 80% ya vumbi duniani hutoka kwenye jangwa la Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, ameongeza Paterson, lakini ina athari ya kimataifa kwa sababu chembe hizo zinaweza kusafiri mamia na hata maelfu ya kilomita katika mabara na bahari.