Kwa nini watu wengi duniani wana mtazamo hasi kuhusu Marekani?
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliochapishwa na Kituo cha Utafiti cha Pew, watu wa Canada na Mexico, majirani wawili wa karibu wa Marekani, wanaitambua nchi hiyo kuwa tishio kubwa zaidi kwao.
Kwa mujibu wa utafiti huo, 59% ya Wacanada na 68% ya Wamexico wanaiona Marekani kuwa tishio kubwa kwa nchi zao. Wakati huo huo, asilimia 55 ya Wacanada na asilimia 37 ya watu wa Mexico wanamtambua jirani yao huyo kama mshirika wao muhimu zaidi kulingana na uchunguzi wa watu duniani kote kuhusu mshirika wao muhimu zaidi na tishio kubwa zaidi. Takwimu hizi zinatokana na uchunguzi wa maoni ya watu duniani kote kuhusu mshirika muhimu zaidi na tishio kubwa zaidi.
Inaonekana kwamba Canada na Mexico, majirani wawili wa kaskazini na kusini wa Marekani, ambao pia walishiriki katika makubaliano ya NAFTA na Marekani, na kimsingi wanatambuliwa kuwa washirika wakubwa wa kibiashara wa Washington, hazijaridhishwa na utawala wa Trump kutokana na sera na hatua za Rais huyo mwenye utata wa Marekani, ambaye amelenga uhusiano wa kibiashara na nchi hizi mbili na hata kutishia umoja wa ardhi ya Canada. Kimsingi nchi mbili hizo zinaitambua Marekani kuwa tishio kubwa kwao.
Canada na Mexico ziko chini ya mashinikizo makubwa kutoka kwa Trump ya kuongeza ushuru kwa bidhaa zao zinazoingizwa Marekani, na kwa upande mwingine, Trump, bila ya kuzingatia au kuheshimu kanuni na sheria za kimataifa, ameitaka Canada kuungana na Marekani kama jimbo la 51 la nchi hiyo.
Kwa upande mwingine, amri za utendaji za Trump za kukabiliana na wahamiaji wanaoingia nchini humo kutoka mpaka wa kusini mwa Marekani (yaani mpaka wa Marekani na Mexico), pamoja na kufukuzwa kwao kwa kutumia mabavu, vimechochea mvutano kati ya Mexico na Marekani. Yote hayo yamewafanya watu wa Canada na Mexico wawe na maoni hasi na mtazamo mbaya sana kuhusu Marekani, wakiiona kuwa tishio kubwa zaidi kwa nchi zao.
Hapo awali, matokeo ya uchambuzi wa data ya kampuni ya ujasusi wa biashara ya Marekani yalionyesha kuwa umaarufu wa Marekani umeshuka sana na kuwa hasi duniani kote baada ya Donald Trump kurejea ikulu ya White House, huku nafasi ya China ikipanda juu. Tovuti ya habari na uchambuzi ya Axios inasisitiza kuwa kushuka kwa hadhi ya Marekani kuna gharama za kiuchumi kwa nchi hiyo, ikibainisha kuwa hali hiyo imeambatana na kupungua kwa watalii kutoka nje ya nchi na hata kushuka kwa thamani ya sarafu ya dola kutokana na sera za Ikulu ya Rais wa Marekani. Axios imesisitiza kwamba bado kuna uwezekano wa kuporomoka zaidi hadhi na umaarufu wa Marekani duniani.
Vilevile ripoti ya Kielezo cha Mtazamo wa Demokrasia 2025 (Democracy Perception Index 2025) ilionyesha kupungua kwa umaarufu wa Marekani duniani, haswa baada ya Donald Trump kurejea Ikulu ya White House. Ripoti hiyo inaonyesha “kuongezeka kwa maoni hasi kuhusu Washington katika zaidi ya nchi 100 zilizochunguzwa.” Kwa mujibu wa ripoti hiyo, iliyokusanywa na Muungano wa Demokrasia, idadi kubwa zaidi ya wahojiwa 110,000 walitoa maoni hasi kuhusu Marekani, suala ambalo linaonyesha kupungua sana kwa umaarufu wa serikali ya Washington ikilinganishwa na mwaka jana. Kupungua huko kulionekana zaidi katika Umoja wa Ulaya, ambao awali Trump aliutaja kuwa "aina ya ufisadi kwa Marekani." Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza China imeitimulia kivumbi Marekani kwa umaarufu duniani, na imepata maoni chanya katika maeneo mengi isipokuwa Ulaya.
Kwa mujibu wa chunguzi za maoni za hivi karibuni, ukiwemo uchunguzi wa maoni wa Chuo Kikuu cha Quincy, Wamarekani wengi pia wana mtazamo hasi kuhusu sera za ndani na nje za Trump. Sababu ya jambo hilo ni kushindwa kwake kutekeleza ahadi alizotoa, kwanza, katika nyanja za ndani na nje ya nchi, na pili, kuongezeka kwa migawanyiko ya ndani nchini Marekani na migawanyiko ya jamii ya Marekani kuhusu sera za Trump, pamoja na kuongezeka kwa hitilafu kati ya Marekani na washirika wake na kushadidi mivutano kati ya madola hasimu hasa China.
Bila ya kuzingatia kuporomoka kwa hadhi na nguvu ya Marekani duniani, Trump amefanya juhudi zisizo na tija za kuwatisha wapinzani wa Marekani na hata washirika wake kwa ajili ya kuwalazimisha wakubali matakwa yake na kushikamana na malengo na sera za Washington.
Hata hivyo, hakufanikiwa kufikia malengo yake. Kwa sasa anacheza tu nafasi ya rais anayeonekana kidhahiri kuwa na nguvu anayetaka kila mtu amtii na kusalimu amri mbele yake, lakini kinyume chake, amepunguza sana nguvu laini ya Merekani duniani na kudhihirisha taswira yake mbaya na ya kuchukiza kwenye jukwaa la kimataifa kwa mbinu yake ya mabavu inayozingatia sera ya "amani kupitia nguvu".